Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba.
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia,
January Makamba (pichani), amesema vyama vya siasa vya CCM na
vunavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vinachimbiana kaburi na
kusubiri mwingine kumzika mwenzake katika uchaguzi mkuu ujao.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa tawi la Jumuiya ya Umoja wa
Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) la Karume mjini hapa juzi, alisema
uchaguzi mkuu wa mwaka huu vyama hivyo vimeandaliana kaburi na yeyote
atakayemuwahi kumuua mwenzake atamzika.
“Uchaguzi wa mwaka huu ni muhimu sana kwa CCM na Ukawa kutokana na
wote kuchimbiana kaburi na kila atakayewahi atamfukia mwenzake na
kukamilisha adhima ya kuingia Ikulu,’ alisema Makamba.
Aidha, Makamba alisema tabia ya wanasiasa kupita kuomba kura
vyuoni, misikitini na makanisani, inaonyesha nia mbaya ya kutaka
madaraka kwa namna hiyo.
Alisema baadhi ya makada wamekuwa wakizunguka katika taasisi za
dini, kwa waendesha bodaboda na machinga ili kuwarubuni waweze kutoa
matamko ya kuwa wanafaa kuongoza nchi.
Alisema joto la kisiasa nchini kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba
mwaka huu, limekuwa kubwa kwa CCM na Ukawa kabla ya hata muda wa kufanya
kampeni haujaanza.
Aidha, Makamba alisema anapingana na baadhi ya watu wanaodai kuwa vijana hawafai kukabidhiwa madaraka makubwa ya kuongoza nchi.
“Nashangaa kuona vijana wengi wanakatishwa tamaa kuwa hawawezi
kuwania nafasi nyeti, dhana hiyo ni mbaya sana na haipaswi kuendelea
kuwapo,” alisema.
Makamba ni mmoja wa makada wa CCM waliotangaza kuwania kuteuliwa na chama hicho kugombea urais uchaguzi mkuu ujao.
إرسال تعليق