Babu amtetea binti aliyekamatwa Kenya, Ni Mtanzania anayedaiwa kutaka kujiunga na Al Shabaab, Alitoroka chuoni Sudan wiki moja kabla ................

Ummul- Khayr Sadri Abdulla.
  Ni Mtanzania anayedaiwa kutaka kujiunga na Al Shabaab� Alitoroka chuoni Sudan wiki moja kabla ya kukamatwa.

Sakata  la msichana wa kitanzania, Ummul- Khayr Sadri Abdulla (19), anayedaiwa kutaka kujiunga na kikundi cha ugaidi cha Al-Shabaab, linazidi kuchukua sura mpya baada ya madai kuwa alitoroka  chuoni Sudan wiki moja kabla ya kukamatwa nchini Kenya.
Binti huyo mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kimataifa Afrika kilichopo Sudan, aliyekuwa akisomea udaktari mwaka wa tatu, kabla ya kukamatwa Machi 30, mwaka huu, alikuwa ameshatoroka chuoni  hapo tangu Machi 22 na ndugu zake walikuwa wanamtafuta.
Akizungumza na NIPASHE Jumapili, babu wa binti huyo, Nassor Said Nofli, alisema kuwa taarifa za kupotea zilitolewa na dada yake mkubwa, Sumaiyya Sadri Abdulla (20), ambaye pia anasomea udaktari mwaka wanne katika chuo hicho.
Anasema familia ilishtushwa na taarifa za kupotea kwa mtoto wao baada ya dada yake kumkosa chuoni hapo.
Nofli alisema ilipofika Machi 23, siku ya Jumatatu hakuonekana darasani wala hosteli (bweni) huku dada yake akiendelea kumtafuta.
Anaendelea kusimulia kuwa ilipofika siku ya Jumanne ilitolewa taarifa kwa baba yake aliyeko Oman kikazi, Dk. Sadri Abdulla Said, pamoja na ndugu wengine waliopo Pemba, Unguja na Dar es Salaam.
Hata hivyo, baba wa mtoto huyo aliwajulisha kuwa atasafiri Machi 25 kuelekea Sudan ili kusaidia kumtafuta.
Alisema kuwa tarehe ambayo baba yake alipanga kusafiri, alikosa hati ya kusafiria na kuahirisha safari hadi alipopata hati ya kusafiri Machi 27.
“Hizi taarifa za kupotea kwa binti yetu zilitushtua na ilitulazimu kuomba maombi maalum ya kumuombea “Dua” ili aweze kuonekana na akiwa salama kwa sababu Sudan kama unavyoielewa ni nchi yenye matatizo ya kivita ,” alisema.
Nofli alisema taarifa za kukamatwa kwa mtoto wao wamezisikia kupitia vyombo vya habari. Alisema wanavishukuru vyombo vya dola kwani familia ilikuwa inamtafuta na hawakujua alipo.
Alisema kama asingekamatwa inaelekea angejiingiza katika vitendo viovu ambapo familia ingeweza kumkosa binti huyo.
“Kitendo cha polisi kumkamata imetusaidia na pia wamesaidia kumuokoa yule mtoto kutokujiingiza kwenye hicho kikundi kwani angeweza kuuliwa ama kupotea katika kundi hilo,” alisema. 
Alieleza kuwa mbali na binti wao kuendelea kushikiliwa na polisi, wanaamini kuwa vyombo vya sheria vitatenda haki.
Nofli alisema anachokitambua ni kwamba binti huyo alikuwa bado hajajiunga na kikundi hicho, hivyo familia ina imani haki itatendeka.
“Familia kwa ujumla tunashukuru kukamatwa kwake kwani ni heri kwake na kwetu kwa kumuokoa katika tukio hilo tunaamini haki itatendeka,” alisema na kuongeza:
“Ninavyoona mimi huyu mjukuu wangu hana kesi ya kujibu kwa kuwa bado hakuingia katika kundi hilo la ugaidi na ninaamini polisi inamshikilia ili kuwakamata magaidi wa kweli.”
Kadhalika alisema jambo lingine lililoishtua familia yake ni pale vyombo vya habari vilivyoeleza kuwa wazazi wa binti huyo ni wahadhiri wa chuo hicho ambacho watoto hao wanasoma jambo ambalo si la kweli.
Alisema jambo hilo limewashtua kwa kuwa linaonekana kuwa  wazazi hao wamehusika katika kumsukuma mtoto wao kutaka kujiingiza katika vikundi hivyo viovu.
Aidha akizungumzia madai ya binti huyo kutaka kuolewa na askari mmojawapo wa kigaidi, alisema ndoa hiyo wasingeitambua kwa kuwa inakwenda kinyume na sheria za ndoa katika uislamu.
Hata hivyo, Taarifa za awali zilionyesha kuwa, binti huyo akiwa na wenzake wawili, Khadija Abubakari Abdulkadir na Maryam Said Aboudall, walikamatwa katika jimbo la El -Wak mpakani mwa Kenya na Somalia.
Inaelezwa pia binti huyo alikuwa katika harakati za kuvuka mpaka na kuingia Somalia kwa lengo la kujiunga na kikundi cha ugaidi na baadaye kuondoka kutoka Mogadishu kwenda Syria kujiunga na kikundi cha kiislamu kinachojulikana kama ISIS ambapo angeolewa na wapiganaji wa kikundi hicho.
Hata hivyo, taarifa kutoka kwa Kamishna wa Polisi Jimbo la El –Wak, Nelson Marwa, zinaonyesha kuwa wasichana hao watatu walikuwa wanakwenda Somalia kupata mafunzo ya kigaidi na baadaye kufanya mashambulizi ya kujitoa mhanga.
NIPASHE ilizungumza na Mhadhiri wa Sheria na Shariah  kutoka Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Morogoro, Tawaqal Hussein, ambaye alisema kwa mujibu wa dini ya kiislamu hakuna ndoa kama hizo na kwamba wanaofanya hivyo ni kosa kubwa mbele ya Mungu.
Alisema sababu ya kutotambulika kwa ndoa hiyo ni moja ya masharti yanayotakiwa kufanyika ni kuwepo na ridhaa kutoka upande wa wazazi wa kiume kutoka kwa mtoto huyo wa kike.
Mkurugenzi wa Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC), Dk.Hellen Kijo Bisimba, alisema kama alikwenda kuolewa haina haja ya kukamatwa kwani suala la ndoa lipo kijamii.
Lakini akaongeza kwa kusema kuwa endapo atakuwa anakwenda kujiunga na kikundi hicho cha ugaidi na uthibitisho ukapatikana ana haki ya kushtakiwa.
"Masuala ya kuolewa ni ya kijamii na kila mtu ana haki ya kuolewa na mtu yoyote hata Osama alioa wake wawili, hapo kinachotakiwa ni kuangalia kama huyo msichana anakwenda kufanya ugaidi au la maana mimi nilisikia kama huyo msichana anataka kujiunga na hicho kikundi cha kigaidi, lakini kama anakwenda kuolewa ina maana familia ina taarifa," alisema Bisimba.
Kwa upande wake, Profesa Abdallah Safari alisema sheria inaruhusu mtu kuolewa na mtu yeyote na kwamba kuolewa na gaidi sio kosa, hivyo kosa litajitokeza endapo mtu anakwenda kushirikiana naye katika kufanya ugaidi.
"Hivi ni watu wangapi wanaolewa na wezi ama jambazi na hata mafisadi wa Escrow, uovu wa mtu unabaki pale pale huwezi kumpa mtu mwingine," alisema Profesa Safari.
Profesa Safari alisema kila nchi ina sheria zake za ugaidi na endapo ikibainika alikwenda kufanya vitendo hivyo atashitakiwa kwa mujibu wa sheria ya ugaidi ya nchini Kenya.
Aliyekuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS),  Francis Stolla, alisema kimsingi katika masuala ya ndoa hakuna kuchaguliana kuolewa na gaidi au la.
Alisema ndoa ina masharti yake ambayo yanatakiwa kufuatwa hata kama ni mtuhumiwa una haki ya kufunga ndoa.
"Ndoa hazivunjwi kwa sababu ya kutiwa hatiani, kosa litajitokeza kama mwanaume huyo atakwenda kushirikiana katika vitendo vya ugaidi," alisema.
Hata hivyo, mpaka sasa wasichana hao bado hawajafunguliwa mashtaka yoyote japo mahakama ya nchini humo imeliruhusu jeshi la polisi kuwashikilia kwa siku 20 kwa ajili ya upelelezi. 
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

Previous Post Next Post