Mh.Bernard Membe
KATIKA mfululizo wa makala hizi zinazochambua wasifu wa wanasiasa
wanaotarajiwa kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu 2015, leo
‘tunammulika’ Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Bernard Camillius Membe ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mtama mkoani
Lindi, Kusini mwa nchi yetu.
Kama tutakavyoona katika uchambuzi huu, huyu ni mgombea mwenye
historia fupi lakini yenye kujaa weledi katika siasa za Tanzania na
kimataifa, hii ni kwa sababu alikuwa shushushu, hivyo mambo yake mengi
kuwa ya siri.
Alizaliwa wapi na lini?
Bernard Camillius Membe alizaliwa Novemba 9, 1953 katika Kijiji cha
Rondo Chiponda, Wilaya ya Lindi Vijijini, akiwa ni mtoto wa pili katika
familia ya watoto saba wa mzee Camillius Anton Ntanchile na mama Cecilia
John Membe.
Membe alifunga ndoa ya Kikristo na Dorcas Richard Masanche mwaka
1986 na Mungu amewajalia watoto watatu, wawili wa kiume na mmoja wa
kike.
Kimaisha Membe hakukulia mjini, alizaliwa na kukua akiwa kijijini
kama Watanzania wengi waliokulia huko walivyo, hivyo anajua tabu
wanayopata wanavijiji kwa sababu alizaliwa katika kijiji ambacho
hakikuwa na zahanati na maji yalikuwa shida, alilazimika kutembea
kilometa nyingi kuyafuata.
Baba yake alikuwa mwindaji aliyelazimika kuwa hivyo akiwa bado mtoto
mdogo miaka kama mitano hivi, wakiwa shambani, Camillius Anton Ntanchile
alishuhudia simba akimnyatia na kisha kumdaka mama yake (Bibi yake
Bernard) na kutokomea naye, na walikuja kupata baadhi tu ya viungo vya
mwili wake.
Kitendo hicho kibaya kilimfanya Camillius akawa na ndoto ya kumiliki
bunduki na kuwa mwindaji na akafanikiwa alipokua mkubwa hivyo basi kama
wanasiasa wengine wanavyoitwa ‘Mtoto wa Mkulima’, Membe anaweza
kupachikwa jina la Mtoto wa Mwindaji!
Baba yake alifariki dunia mwaka 1987 kwa ajali ya kulipukiwa na
bunduki pajani baada ya kuvuja damu nyingi akiwa porini. Kwa maelezo ya
Membe, hii ndiyo hali iliyomchochea kupigania uwepo wa hospitali ya
wilaya katika jimbo lake la uchaguzi.
USOMI NA REKODI ZITAMSAIDIA KUWA RAIS 2015?
Kwa kiasi kikubwa, Membe amefuata mtiririko wa kawaida katika kusoma
kwake, elimu ya msingi aliipata katika Shule ya Msingi Rondo Chiponda
mwaka 1962 hadi 1968.
Shule ya sekondari alisomea katika Seminari ya Namupa (1969 hadi
1972), akajiunga na Itaga Seminari Tabora kwa kidato cha tano na sita
(1973 hadi 1974.)
Maandiko mbalimbali niliyowahi kuyasoma yanaeleza kwamba Membe aliwahi kusomea upadri kwa miezi kadhaa.
Baada ya kumaliza kidato cha sita mwaka 1974, Membe alijiunga kwa
mujibu wa sheria mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa muda wa
mwaka mmoja.
Alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (1981/82), alisomea
shahada ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma akitokea Ofisi ya Rais
alipokuwa ameajiriwa.
KUMBE NI ‘KICHWA’
Matokeo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yanaonyesha kwamba Membe
alifaulu vizuri kwa kiwango cha kupata GPA ya 4.1, huu ni ufaulu wa juu
sana, alipewa barua ya ajira ya uhadhiri wa chuo kikuu hicho katika
ngazi ya uhadhiri msaidizi (tutorial assistant), alishindwa kujiunga kwa
sababu mwajiri wake, ikulu, alikataa.
Bernard Camillius Membe anayo pia shahada ya uzamili katika Uhusiano
wa Kimataifa aliyoipata kutoka Chuo Kikuu cha Johns Hopkins nchini
Marekani mwaka 1992.
MSAIDIZI WA MKURUGENZI
Akiwa kachero ikulu alipanda ngazi kadhaa na hata kuwa msaidizi wa
waliopata kuwa wakurugenzi wakuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Dk. Hans
Kitine na Apson Mwang’onda.
Baadaye Membe alipelekwa ubalozi wa Tanzania nchini Canada kama
Mwambata wa Ubalozi (Minister Plenipotentiary), alidumu katika nafasi
hiyo hadi mwaka 2,000 alipoamua kugombea ubunge, akashinda na kuwa
mbunge wa pili wa Jimbo jipya la Mtama, Lindi akimrithi Masoud Ally
Chitende.
ALIVYOMKAMPENIA JK
Katika kampeni za urais za mwaka 2005 ndani na nje ya CCM, Membe
alifanya kazi kwa karibu na akina Edward Lowassa na Apson katika
kuhakikisha kwamba Rais Jakaya Mrisho Kikwete anapitishwa kuwa mgombea
na hatimaye kushinda katika uchaguzi wa urais.
Baada ya Rais Kikwete kushinda uchaguzi wa mwaka 2005 alimteua Membe
kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini nafasi aliyoshikilia kati ya
Oktoba 2006 na Januari 2007, na baadaye Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani
kati ya Januari 2006 na Oktoba 2006.
Baada ya kuteuliwa kwa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Dk. Asha-Rose Migiro kuwa Naibu Katibu Mkuu wa
Umoja wa Mataifa, Rais Kikwete alimteua Membe kuchukua nafasi yake na
anaishikilia hadi leo
UTATA WAKE
Membe aliitangazia dunia kupitia Bunge letu Mei 27, 2014 kwamba waasi
wa kikundi cha M 23 huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kuwa
walikuwa ni raia wa Rwanda na walikuwa wakifadhiliwa na Serikali ya
Rwanda. Hii ilileta shida kidiplomasia. Pia alilaumiwa kuhusiana na
matakwa yake ya kuruhusu uraia pacha na aliungwa mkono na Rais Kikwete,
jambo ambalo Baba wa Taifa, mwalimu Julius Nyerere alilipinga.
UADILIFU WAKE
Bernard Membe ni kati ya viongozi wachache katika serikali ya CCM wanaotajwa kwamba ni waadilifu.
Mapema katika Bunge la mwaka 2001/2002, paliibuka kashfa kubwa
ikimhusisha aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora, Dk.
Hans Kitine. Katika kashfa hiyo ilidaiwa kwamba Dk. Kitine alikuwa
ametumia fedha za serikali kwa kumtibu mke wake, Saada Mkwawa Kitine,
nje ya nchi kwa kiwango cha dola za Kimarekani 63,000.
Ni katika hatua hii ambapo Bernard Membe alisimama Bungeni akamwaga
nyaraka zinazoonyesha jinsi fedha zilivyotumwa kwenye akaunti binafsi ya
mama Kitine badala ya kutumwa katika akaunti ya ubalozi. Dk Kitine
ilibidi aachie ngazi serikalini.
Membe ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM aliyeshinda mwaka
2012 na hivi karibuni amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri
wa Nchi za Jumuiya ya Madola (CMAG).
Kiongozi huyu anajitambulisha kwa taswira ya uadilifu na kwa kweli ni
vigumu kumhusisha na kashfa yoyote iliyotokea hapa nchini, anajivunia
rekodi ya kuipaisha Tanzania katika anga za kimataifa kidiplomasia hivyo
ukilinganisha na wagombea wengine, huyu anaweza ‘kupeta’ ikiwa turufu
yake itakubaliwa na vikao vya juu vya CCM awanie urais.

إرسال تعليق