Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Dar es Salaam
kinakabiliwa na kashfa ya kushirikiana na kliniki binafsi za raia wa
Korea Kaskazini, zinazodaiwa kuuza dawa zinazoathiri afya na maisha ya
watu.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa miezi kadhaa, umepata
taarifa za vyanzo tofauti zinazoelezea upungufu wa kitabibu kwa dawa
zinazotolewa na kliniki hizo, hususani zilizopo Temeke, Magomeni na
Kariakoo jijini humo, lakini serikali haijachukua hatua zozote za
udhibiti.
Taarifa za hivi karibuni zinaeleza kuwa baada ya kufichuliwa kwa
upungufu huo, wamiliki wa kliniki hizo wanatumia muda mwingi kutoa
taarifa kwa wagonjwa wanaofika, wakikanusha kuhusu upungufu na madhara
yanayotajwa kuwapo kwenye dawa zao. Pia wanakitumia CCM kama kinga ama
ushawishi kwa umma kwamba utendaji wao unakidhi matakwa ya sheria na
kanuni za tiba.
Gazeti hili limepata nakala ya barua moja iliyoandikwa na Wizara ya
Afya na Ustawi wa Jamii kwenda CCM mkoa wa Dar es Salaam, kujibu ombi
la kutaka kliniki hizo kuruhusiwa kutoa pia huduma za tiba za kisasa.
Barua hiyo (kumbukumbu namba na ofisa aliyeisaini tunavihifadhi kwa
vile hajapatikana kuielezea), ilionyesha kujibu barua ya CCM mkoa wa
Dar es Salaam ikiwa ni mmiliki wa kliniki hiyo.
Pamoja na mambo mengine, ilieleza ombi la CCM kutaka kampuni ya
Maibong-Sukidar inayomilikiwa na chama hicho kutoa tiba kutumia dawa za
kisasa na asilia kutoka Korea.
Barua hiyo ya wizara inaeleza msimamo wake kwamba kliniki hiyo
ilipewa kibali kutoa tiba asilia kutoka Korea na kwamba kama kulikuwa na
hitaji la kutoa tiba za kisasa, ilipaswa kuwasilisha vielelzo
vinavyothibitisha kuwa madaktari na wafamasia wake wana uelewa kuhusu
tiba za kisasa.
Hata hivyo, bado haijathibikika kama agizo hilo la wizara lililotolewa mwaka 2008 lilifanyiwa kazi na CCM au kliniki hiyo.
Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Abilah Mihewa, amethibitisha
chama hicho kuingia ubia na Wakorea Kaskazini katika biashara ya kliniki
hizo, ingawa miongoni mwa makubaliano yaliyofikiwa na uongozi uliopita
yanafanyiwa kazi.
Mihewa alisema kwa upande wa Temeke, CCM ilikubaliana na Wakorea
hao kuwekeza kwenye ardhi yake na kwamba CCM haihusiki na shughuli za
uendeshaji na utoaji huduma za afya.
Hata hivyo, Mihewa alisema kliniki iliyopo Magomeni Mikumi, uongozi
wake bado haujapata uthibitisho wa namna CCM inavyoshiriki ikiwa ni kwa
umiliki wa ardhi pekee au pamoja na majengo.
Alisema hali hiyo inatokana na hatua za makubaliano ya biashara
hiyo kufanywa na uongozi uliopita ambapo mpaka sasa ofisi yake
inaendelea kulishughulikia suala hilo ili kupata ufumbuzi wa kudumu.
HOFU YA KUPOTEZA KURA
Sakata hilo linadaiwa kuwa huenda likaibua madhara kama upofu,
kupoteza fahamu, mwili kulegea na kuwa kiziwi kwa watu baada ya muda
mrefu, zinazidi kukiweka chama hicho katika hatari ya kutoungwa mkono
katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu. Hali hiyo inatokana na jinsi
CCM, serikali na mamlaka husika zilivyoshindwa kushughulikia kero
mbalimbali za kijamii na kusababisha kupoteza viti vingi wakati wa
uchaguzi wa serikali za mitaa.
Waziri wa Afya na Ustawi na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid na
Meneja Ukaguzi na Udhibiti wa Dawa na Vipodozi wa Mamlaka ya Chakula na
Dawa (TFDA) kanda ya Mashariki, Emmanuel Alphonce, hawakupatikana
kuelezea sakata hilo.
Lakini Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Hiiti
Sillo aliwahi kuliambia gazeti dada la The Guardian hivi karibuni kuwa
ukaguzi dhidi ya tuhuma hizo ungefanywa na mamlaka hiyo, lakini hakuna
taarifa kuhusu utekelezaji wake.
Post a Comment