Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jana
kilizindua mkakati wake wa ushindi “Hakuna kulala, hakuna kula mpaka
kieleweke” katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba kwa kufungua mafunzo
yatakayoendeshwa nchi nzima kwa viongozi wa vyama na Serikali za Mitaa.
Katika mkakati huo, chama hicho kimeigawa nchi
katika kanda 10 za utekelezaji huku kikijipanga kuimarisha nguvu zaidi
katika Jiji la Dar es Salaam lenye idadi kubwa ya wapigakura.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema
wakati wa uzinduzi wa mkakati huo kitaifa jijini hapa kuwa watafundisha
viongozi wote wa chama hicho na watangaza nia, mbinu za uongozi bora na
namna ya kushinda.
Mbowe alisema mpango huo wa mafunzo ni sehemu ya
utekelezaji wa maazimio ya chama kwa kuwa hawawezi kushika Serikali Kuu
na Serikali za Mitaa bila kuwa na viongozi bora na weledi.
Alisema Chadema kitakwenda katika kanda zote,
majimbo ya kichama 242, kata 4,852, matawi 22, 749, misingi 64,803 na
kuwafikia viongozi 224,287 na timu zote za mafunzo zimeshatawanyika nchi
nzima.
“Tunawafundisha viongozi wetu walio tayari ndani
ya chama au Serikali za Mitaa namna ya kutekeleza wajibu wao. Lakini
tunawaimarisha wanaokusudia kugombea nafasi mbalimbali kuwa wagombea
wazuri zaidi, kuandaa ajenda za chama na namna ya kukamata madaraka kwa
kuwa safari ya kushika Dola 2015 haina kizuizi,” alisema Mbowe huku
akishangiliwa.
Kuahirisha uchaguzi
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na mamia ya
viongozi na watia nia wa Kanda ya Pwani ya chama hicho, Mbowe aliitaka
Serikali kutojaribu kabisa kuahirisha Uchaguzi Mkuu kwa sababu ya
kusuasua kwa uandikishaji wa daftari la kudumu la wapigakura kwa kutumia
teknolojia ya Biometric Voters Registration (BVR) akitishia kuwa ‘moto
utawaka’.
Alisema Ukawa hawakusema chochote wakati wa Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilipoahirisha Kura ya Maoni ya Katiba
Inayopendekezwa kwa kuwa ilikuwa batili na ilianzishwa kwa masilahi ya
Serikali na aliahirishwa na wao wenyewe.
Aliitaka Serikali kuharakisha uandikishaji wa
daftari la kudumu la wapigakura kwa kuwa imesalia miezi mitatu na nusu
kabla ya kuanza kwa kampeni za Uchaguzi Mkuu hapo Agosti.
Alisema tarehe ya kupiga kura ambayo ni Jumapili
ya Oktoba ilifahamika tangu awali kwa kuwa ni ya kikatiba lakini mpaka
sasa uandikishaji unasuasua katika Mkoa wa Njombe wenye wapiga kura
340,000 ambao alisema hawafiki hata nusu ya waliopo Jimbo la Ubungo.
“Wanasubiri kama walivyofanya kwenye kuahirisha
Kura ya Maoni na ili waseme ‘ndugu Watanzania kwa kuwa tumechelewa
kuandikisha wapigakura tunaomba Bunge lako tukufu liongezee muda kwa
Serikali ya awamu ya nne’... mtakubali?” aliwahoji wafuasi hao na
kujibiwa “Hapanaaaa”
Post a Comment