Ukerewe. Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) kimeweka
mkakati utakaowafanya makada wake wavamie majimbo yanayoshikiliwa mapema
na CCM, huku wakichelea kuingia kwenye majimbo yaliyo chini ya chama
hicho kikuu cha upinzani.
Mkakati huo ulitangazwa jana na Mwenyekiti wa
Chadema, Freeman Mbowe wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika
kwenye Uwanja wa Mongella mjini hapa, mkutano ambao ulifurika maelfu ya
watu.
Mbowe alitangaza kupiga marufuku wanachama wa
Chadema kuanza kutangaza nia kwenye majimbo ambayo wenzao wanayashikilia
hadi hapo Bunge la Jamhuri ya Muungano litakapovunjwa.
Lakini alisema wanachama wa Chadema wanaruhusiwa
kuanza purukushani kwenye majimbo ambayo yanashikilia na vyama vingine
hasa chama tawala cha CCM ambacho kinashikilia majimbo mengi.
“Naomba ifahamike Chadema ni zaidi ya ubunge,
tunahitaji amani na siyo kuharibu chama. Chadema itasimamisha watu
makini kwenye maeneo yote katika uchaguzi huu,” alisema mwenyekiti huyo
ambaye yuko kwenye ziara ya mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Mbowe ambaye hakugusia suala la Ukawa katika
mkutano huo, alisema kuwa utaratibu utaandaliwa wa kupata wagombea na
kwamba hata waliokuwa wabunge, wasijihakikishie kuwa watapitishwa tena
kwenye maeneo yao wanayoyaongoza sasa.
“Tutakuja na utaratibu mwingine. Hata wabunge wa
Chadema waliokuwa katika maeneo hayo, wasidhani kwamba watabakia hapo.
Tutasimamisha mtu anayekubalika na watu wote, na utaratibu ukiwekwa,
hata aliyekuwa mbunge anaweza kuondolewa,” alisema Mbowe.
Alisema kuwa Chadema inaamini kuwa katika kila eneo kuna mtu wake ambaye ni makini na ni wazi atashinda.
Vyama vinne vya upinzani, Chadema, NLD,
NCCR-Mageuzi na CUF vimekubaliana kusimamisha mgombea mmoja kuanzia
kwenye uchaguzi wa madiwani hadi rais. Vyama hivyo, vilivyo chini ya
mwavuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), vimekubaliana kuwa kila
chama kipate mgombea wake na baadaye vitachambua anayekubalika na wengi.
Ainanga Nec
Akizungumzia mwenendo wa uboreshaji wa Daftari la
Wapigakura, Mbowe alisema Taifa kwa sasa liko kwenye giza nene kutokana
na maandalizi mabovu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi(Nec).
Mbowe alisema kucheleweshwa kwa kazi ya
uandikishaji wapigakura ni sehemu ya njama za CCM kupitia Serikali yake
inayotamani kutumia nafasi hiyo ili kuendelea na hujuma katika Uchaguzi
Mkuu wa Oktoba.
إرسال تعليق