DC ampigia debe la urais Wasira

Mbeya. Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Nyerembe Sabi, amempigia debe Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira, pale alipoeleza kuwa yeye siyo waziri na mbunge tu, bali ni mtarajiwa.
Alisema hayo katika mkutano wake na Watafiti wa Taasisi ya Maendeleo na Utafiti wa Mazao Uyole, uliofanyika mwishoni mwa juma.
Mkuu huyo wa wilaya alitoa kauli hiyo alipokuwa akimkaribisha Waziri Wasira kwenye hafla ya kufunga utafiti wa mbegu bora za viazi mvirigno, uliokuwa ukifanywa na taasisi ya Ari Uyole kwa udhamini wa Nchi ya Ufini (Finland)
Utafiti huo ulianza 2011 na ulimalizika mwishoni mwa juma na wakulima wataanza kutumia mbegu hizo bora katika msimu huu wa kilimo. Mbegu hizo zinatoa tani 18 kwa ekari badala ya tani tano au nane za awali.
“Mheshimiwa Waziri, mbunge ambaye pia ni mtarajiwa’’ alisema mkuu huyo wa wilaya bila kumalizia ni mtarajiwa wa nini na kusababisha watu kuangua kicheko.
Ingawa mkuu huyo wa wilaya hakutaka kusema Wasira anatarajia nini, tayari mbunge huyo wa Bunda amewaambia baadhi ya wanaCCM kuwa anatarajia kugombea urais katika uchaguzi mkuu ujao.
Nia hiyo ya Wasira kuutaka urais, inathibitishwa pia na uamuzi wa CCM kumwadhibu kwa kuanza kampeni mapema, sambamba na makada wengine watano wa chama hicho, akiwamo Bernard Membe, Frederick Sumaye, Edward Lowassa, Januari Makamba na William Ngeleja.
Alipoulizwa na mwandishi kwa nini anaitwa mtarajiwa, Wasira alijibu kwa kifupi, “ Kamuulize DC mwenyewe atakueleza”.
Katika hotuba na mazungumzo yake kwenye hafla hiyo, Wasira hakugusia suala la uchaguzi ama urais bali alijikita zaidi kwenye umuhimu wa suala la utafiti wa mbegu bora kwa manufaa ya wakulima.
Pia Wasira aliwalaumu maofisa kilimo nchini, akisema wameshindwa kazi waliyotumwa na Serikali ya kwenda kubadili maisha ya wananchi wa vijijini kwa kuwaongoza katika kilimo chenye tija

Post a Comment

أحدث أقدم