Mkinga. Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hoseah amesema uchunguzi wa
gharama zilizotumika kujenga kituo kipya cha mabasi cha Kange jijini
Tanga, utakamilika kwa siku 14 kuanzia sasa.
Mradi wa kituo hicho pamoja na eneo la kuegesha
malori ambao umeshakamilika na kuanza kutumiwa, unadaiwa kugharimu Sh10
bilioni ambazo ni mkopo wa Benki ya Dunia.
Hata hivyo, mbali na gharama za ujenzi huo zimezua
malalamiko kutoka kwa wananchi wanaodai kuwa ubora wa kituo hicho
haulingani na thamani halisi ya fedha.
Dk Hosea alisema wananchi wanahisi kwamba mchakato
mzima wa ujenzi huo uligubikwa na rushwa iliyosababisha kujengwa chini
ya kiwango.
Dk Hoseah ambaye alikuwa wilayani hapa kuzindua
jengo la ghorofa moja la ofisi za Takukuru lililogharimu Sh 1.2 bilioni,
alisema malalamiko hayo yapo mezani kwake na alishatuma maofisa wake
kufanya uchunguzi.
Alisema ataweka bayana kila kilichotumika.
“Nipeni wiki mbili uchunguzi utakuwa umekamilika
na nitampa maelekezo Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Tanga, Aidan Ndomba
naahidi kuchukua hatua za haraka kwa wale watakaobainika kufanya
ubadhilifu katika ujenzi huu wa stendi ya Kange,” alisema Dk Hoseah.
Mwishoni mwa mwezi uliopita katika Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa
wa Tanga, Mbunge wa Tanga, Omari Nundu alichachamaa akidai kwamba hata
mtu asiyesoma anajua kabisa kwamba kituo hicho hakikujengwa kwa gharama
hiyo.
Nundu alisema ni wazi kuwa fedha zilizotolewa katika ujenzi huo zitakuwa zimeliwa na wajanja.
“Haiwezekani kituo cha mabasi kiwe kimejengwa kwa
Sh6.4 bilioni na maegesho la malori Sh2.6 bilioni, lazima nipewe
maelezo hapa, wananchi hawatawaeleweni,” alinukuliwa akisema Nundu
katika kikao hicho.
Post a Comment