Waziri Mukangara abaini chanzo vijana kujiingiza ugaidi.

Waziri wa Habari, Vijana na Michezo, Dk. Fenella Mukangara.
Waziri wa Habari, Vijana na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, amesema kuwa, kutajwa na kujihusisha vijana wa kitanzania kwenye ugaidi kunatokana na kushawishiwa na kurubuniwa.
 
Wakati Dk. Fenella akitoa kauli hiyo, tayari vijana wa kitanzania wametajwa kuhusika kwenye matukio ya kigaidi, huku mmoja akidaiwa kuwa miongoni mwa wale walioshambulia Chuo Kikuu cha Garissa kilichopo nchini Kenya na kusababisha vifo vya watu 148.
Katika tukio hilo, kijana Rashid Charles Mberesero (21 ) ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tano, katika shule ya Sekondari ya Bihawana iliyopo Dodoma, alituhumiwa kuwa mmoja wa wanamgambo wa Al-Shabaab.
 
Akizungumza na NIPASHE Jumamosi juzi, Dk. Mukangara alisema kuwa, vijana wengi hawana ajira na baadhi yao wamekata tamaa ya maisha.
 
Alisema kutokana na uchanga wao ni rahisi kushawishiwa au kurubuniwa kwenye mambo hayo kwa kuahidiwa fedha nyingi mara wanapokubali.
 
‘Inawezekana kabisa wakajiingiza kwenye makosa haya kwa kushawishiwa au kurubuniwa, ushawishi unatokana na fedha anazoahidiwa,” alisema.
 
Pia alisema kuwa vijana kujiingiza kwenye matukio hayo kunatokana na ukosefu wa maadili.
 
“Wanatakiwa kujitambua wajue nafasi zao kwenye nchi, wanapaswa kufahamishwa ugaidi ni hatari kwao na kwa taifa lao,” alisema na kuongeza:
 
“Kazi kubwa tunapaswa kuifanya kama jamii ni kujua vijana wapo wapi na wanafanya nini,  unajua  wengine wamekuwa wakifanya hivyo kwa sababu ya kuwa na imani fulani, sasa basi wanatakiwa kupewa elimu ili wajitambue na kufahamu nafasi zao kwenye nchi,” alisema.
 
Aidha, alisema jamii inapaswa kutambua kuwa katika kundi moja la vijana, miongoni mwao wapo wenye matatizo ambayo yanapaswa kutatuliwa.
 
Alitoa wito kwa jamii kuhakikisha kuwa maadili yanafundishwa kwao wakati wote ili nchi ipate watu wa kuiendeleza.
 
“Vijana nao wajitambue na waelewe nchi hii haitajengwa na mtu/watu kutoka nje ya nchi bali wao, mnapaswa kujikita katika kutafuta maendeleo kwa kutumia mbinu zilizo sahihi,” alisema.
 
Pia alitoa wito kwa wadau mbalimbali zikiwemo sekta binafsi kuhakikisha, wanakuwa na mbinu mbadala za kutengeneza ajira kwa vijana.

Post a Comment

Previous Post Next Post