Waziri wa Habari, Vijana na Michezo, Dk. Fenella Mukangara.
Waziri wa Habari, Vijana na Michezo, Dk. Fenella
Mukangara, amesema kuwa, kutajwa na kujihusisha vijana wa kitanzania
kwenye ugaidi kunatokana na kushawishiwa na kurubuniwa.
Wakati Dk. Fenella akitoa kauli hiyo, tayari vijana wa kitanzania
wametajwa kuhusika kwenye matukio ya kigaidi, huku mmoja akidaiwa kuwa
miongoni mwa wale walioshambulia Chuo Kikuu cha Garissa kilichopo nchini
Kenya na kusababisha vifo vya watu 148.
Katika tukio hilo, kijana Rashid Charles Mberesero (21 ) ambaye ni
mwanafunzi wa kidato cha tano, katika shule ya Sekondari ya Bihawana
iliyopo Dodoma, alituhumiwa kuwa mmoja wa wanamgambo wa Al-Shabaab.
Akizungumza na NIPASHE Jumamosi juzi, Dk. Mukangara alisema kuwa,
vijana wengi hawana ajira na baadhi yao wamekata tamaa ya maisha.
Alisema kutokana na uchanga wao ni rahisi kushawishiwa au
kurubuniwa kwenye mambo hayo kwa kuahidiwa fedha nyingi mara
wanapokubali.
‘Inawezekana kabisa wakajiingiza kwenye makosa haya kwa
kushawishiwa au kurubuniwa, ushawishi unatokana na fedha anazoahidiwa,”
alisema.
Pia alisema kuwa vijana kujiingiza kwenye matukio hayo kunatokana na ukosefu wa maadili.
“Wanatakiwa kujitambua wajue nafasi zao kwenye nchi, wanapaswa
kufahamishwa ugaidi ni hatari kwao na kwa taifa lao,” alisema na
kuongeza:
“Kazi kubwa tunapaswa kuifanya kama jamii ni kujua vijana wapo wapi
na wanafanya nini, unajua wengine wamekuwa wakifanya hivyo kwa sababu
ya kuwa na imani fulani, sasa basi wanatakiwa kupewa elimu ili
wajitambue na kufahamu nafasi zao kwenye nchi,” alisema.
Aidha, alisema jamii inapaswa kutambua kuwa katika kundi moja la
vijana, miongoni mwao wapo wenye matatizo ambayo yanapaswa kutatuliwa.
Alitoa wito kwa jamii kuhakikisha kuwa maadili yanafundishwa kwao wakati wote ili nchi ipate watu wa kuiendeleza.
“Vijana nao wajitambue na waelewe nchi hii haitajengwa na mtu/watu
kutoka nje ya nchi bali wao, mnapaswa kujikita katika kutafuta maendeleo
kwa kutumia mbinu zilizo sahihi,” alisema.
Pia alitoa wito kwa wadau mbalimbali zikiwemo sekta binafsi
kuhakikisha, wanakuwa na mbinu mbadala za kutengeneza ajira kwa vijana.
إرسال تعليق