Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima.
Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu
Josephat Gwajima (pichani), anatarajiwa kuhojiwa leo na Jeshi la Polisi
Kanda Maalum Dar es Salaam katika Kituo cha Polisi cha Kati huku
wasaidizi wake wakisema afya imeimarika na yupo tayari kwa mahojiano
hayo.
Akizungumza na NIPASHE Mwanasheria wa Askofu Gwajima, Paul Mallya,
alisema jana kuwa mteja wake afya yake imeimarika na yupo tayari kwa
mahojiano ya mwisho leo.
“Mteja wangu anaeandelea vizuri, kesho (leo) saa mbili asubuhi
atahojiwa kama maelekezo ya mwisho ya Jeshi la Polisi yalivyomtaka aende
kuhojiwa,” alisema Mallya.
Hata hivyo, Mallya alisema hafahamu kuwa Askofu Gwajima ataongozana
na msafara wa watu wangapi huku akisistiza kuwa anachofahamu ni kuwa
mteja wake atafika kituo cha polisi cha kati kwa ajili ya mahojiano.
Naye mmoja wa wasaidizi wa karibu wa Askofu ambaye hakutaka jina
lake litajwe gazetini, alilieleza NIPASHE jana kuwa afya ya kiongozi
huyo wa kiroho imeimarika na atakwenda katika mahojiano kama
ilivyopangwa, lakini alisema hafahamu ni msafara wa watu wangapi
utakaomsikdikiza.
Jitihada za kumtafuta kupitia simu yake ya mkononi Kamanda wa
Polisi wa kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, kuzungumzia
jinsi polisi walivyojipanga kiulinzi endapo Askofu Gwajima atakwenda
kituoni hapo na msafara wa waamini wake, simu yake haikupokelewa.
Aprili 2, mwaka huu Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam
lilishindwa kumhoji Askofu Gwajima kutokana na kutoridhika na mwenendo
wa afya yake, hali iliyomlazimu kuagizwa kurudi tena leo kwa ajili ya
mahojiano hayo.
Wakili Mallya, alisema Askofu Gwajima atakwenda Polisi tena
kuhojiwa kutokana na mtu aliyetambulika kwa jina la Abubakar Yusufu,
mkazi wa Kiluvya, wilaya ya Kisarawe, mkoa wa Pwani, kufungua kesi ya
jinai polisi akilalamika kukwazwa na lugha iliyotumiwa na askofu huyo
dhidi ya Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam,
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.
Alisema Yusufu alifungua mashtaka hayo kutokana na picha ya video
aliyoiona kwenye mitandao ya kijamii inayomuonyesha Askofu Gwajima
akitumia lugha ya matusi kumkashifu Askofu Pengo ambayo kisheria
ni kosa.
Machi 26, mwaka huu, Jeshi la Polisi Kanda hiyo lilimwamuru Askofu
Gwajima kujisalimilisha polisi kwa tuhuma za kumkashifu Kardinali Pengo.
Machi 27, Askofu Gwajima alijisalimisha kituo hicho, lakini wakati
akihojiwa alizimia akiwa chumba cha mahojiano kisha kukimbizwa katika
Hospitali ya TMJ kwa matibabu.
Jumanne ya wiki iliyopita aliondolewa TMJ na kupelekwa katika Kituo
cha Polisi Oyesterbay na kuachiwa bila masharti, lakini alielekezwa
kuripoti Alhamisi iliyopitwa katika Kituo cha Polisi Kati.
Post a Comment