Rais
Mstaafu, Benjamin Mkapa, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo
pichani) muda mfupi baada ya kutoa mhadhara kwa wanafunzi wanaochukua
mafunzo ya ulinzi na usalama katika Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC),
kilichipo Kunduchi, jijini Dar es Salaam jana. Mada aliyozungumza ni
‘Vita ya tatu ya Dunia’ ambayo chanzo chake kikubwa ilikuwa ni matatizo
ya kiuchumi na uongozi mbovu. Picha na Khalfan Said
Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, amezipa angalizo nchi
za Kiafrika kukuza uongozi bora na kuachana na mikataba mibovu isiyojali
ustawi wa wananchi kwa kuwa inaweza kuzipeleka katika vita.
Miongoni mwa mikataba ambayo amesema kuwa ni mibovu na isiyofaa,
hivyo iepukwe ni wa Kiuchumi baina ya Mataifa ya Afrika, Caribbean na
Pacific (EPA), ili kuepusha vita, ambayo kwa sasa itakuwa ni ya
kiuchumi.
Aidha, ametaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC)
lifumuliwe ili kuongeza nchi nyingine ambazo zinastahili kuingia kwa
sasa.
Rais huyo wa awamu ya tatu aliyasema hayo jana jijini Dar es
Salaam, wakati wa mahojiano aliyoyafanya na vyombo vya habari kwenye
Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC), baada ya kutoa mhadhara kwa wanafunzi
wa chuo hicho.
Mkapa alitoa mhadhara kuhusiana na tathmini ya kiuchumi kuelekea vita ya tatu ya dunia.
Mkapa alisema kwa hali ilivyo sasa ni sababu za kiuchumi ndizo
zinazoleta vita, kutokana na uongozi mbaya, njaa na kiu ya baadhi ya
nchi kutaka maliasili za mataifa mengine.
“Hatutarajii kuwa na vita kama ile ya pili ya dunia, kwa sababu
Dunia sasa inamiliki silaha kali kama za nyuklia, zinazoweza kuangamiza
maisha kwa wingi, na ndiyo maana unaona mazungumzo kupunguza silaha za
nyuklia kama yale ya Iran,” alisema.
Alisema ili kuzuia vita kutokea ndani ya nchi, ama kati ya nchi
mbili, ukanda, bara na hata dunia, kuna umuhimu wa serikali zilizoko
madarakani na hasa barani Afrika kuwekeza kwenye uongozi bora na
kuwashirikisha wananchi katika maamuzi ya kidemokrasia, yanayohusu
maisha na rasilimali za nchi zao.
“Ni vizuri kuwa na sera zinazojenga, zisizogawa wananchi katika
misingi ya udini na ukabila, kuhakikisha mikataba inayoingiwa juu ya
rasilimali za nchi inawanufaisha wananchi na si wageni peke yao, na kama
kuna unahitaji wa kuirekebisha, ni bora hilo likafanyika,” alisema.
Alisema mikataba kama ule wa EPA, si ya kuiruhusu kwani mwisho wa
siku itaua juhudi za nchi maskini kuendelea, kwa sababu zinalenga
kuifanya Afrika kuwa soko la bidhaa za Ulaya.
“Mazungumzo juu ya EPA kwa nchi nyingi zilizo kwenye eneo la Sahara
ni kama yamemalizika, kinachosubiriwa sana sana na kuridhiwa na
mabunge, lakini mkataba huu kimsingi haufai kwa nchi zetu za Afrika,”
alitahadharisha Mkapa.
Mkapa alisema: “Iwapo EPA itaridhiwa na mataifa yetu, itakuwa ni
chanzo cha kudhoofisha kilimo chetu, viwanda vyetu, malighafi
hazitasindikwa na maduka yetu yatajaa bidhaa za Ulaya na mwisho wa siku
ajira itakosekana.”
Akizungumzia suala la muundo wa sasa wa UNSC, Mkapa alisema: “Kuna
umuhimu wa kuifumua taasisi hiyo kwa sababu dunia sasa imebadilika,
tofauti na ilivyokuwa wakati inaundwa,” alisema.
Alisema tasisi hiyo inastahili kufumuliwa na kuundwa upya kwa
sababu hivi sasa kuna mataifa ambayo yameendelea sana kiuchumi na
kiuwezo katika dhana za kivita na hivyo kustahili kuwamo ndani yake.
Alisema mataifa hayo yanastahili kuwamo ndani ya taasisi hiyo kwa
sababu ya ushawishi na nafasi yaliyonayo sasa, inayoyafanya yawe na
mchango kwenye maamuzi ya taasisi hiyo.
Taasisi hiyo ina nchi wanachama 15, nchi tano zikiwa ni wanachama
wa kudumu, zenye kura ya turufu na nchi 10 zikiwa si wanachama wa
kudumu.
Nchi wanachama wa kudumu na zenye kura ya turufu ni Marekani, Urusi, Uingereza, Ufaransa na China.
Kumekuwapo na kilio cha siku nyingi cha kutaka chombo hicho
kufanyiwa marekebisho kwa kukipanua na kuzipa nchi nyingine zaidi nafasi
za uwakilishi. Baadhi ya nchi ambazo zinapendekezwa ni Brazil na India
huku ikipendekezwa Afrika kuwakilishwa na Nigeria na Afrika Kusini.
Kwa upande wake, Mkuu wa chuo hicho, Meja Jenerali Gaudens Milanzi,
alisema ujio wa mkuu huyo wa nchi mstaafu, ni faraja kwao kama chuo cha
Taifa cha ulinzi.
“Hii inaonyesha kuwa bado viongozi wetu waliopita wanaendelea
kukienzi chuo, na bado wanaendelea kuchangia mawazo yao kama kawaida
kwenye masuala ya usalama na stratejia nchini na katika dunia kwa ujumla
wake,” alisema Jenerali Milanzi
Post a Comment