Nuzulack Dausen, Mwananchi
Dar es Salaam. Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT - Tanzania, Zitto Kabwe ameweka hadharani utajiri wake akisema ana
fedha taslimu Sh18 milioni na nyumba mbili zenye thamani ya Sh223 milioni
zilizopo Mwandiga, Kigoma.
Zitto alitangaza mali hizo ikiwa ni sehemu ya kutimiza
matakwa ya katiba na kanuni za maadili ya viongozi wa chama hicho
kinachojinasibu kwa kuenzi sera ya ujamaa wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere ya
mwaka 2015.
Kwa mujibu wa fomu hiyo aliyoijaza, Mbunge huyo wa zamani wa
Kigoma Kaskazini (Chadema), hadi
Machi 29, alikuwa pia anamiliki fedha katika
akaunti mbalimbali za benki; CRDB ana Sh5.98 milioni, Dola za Marekani 188
(Sh347,000) na Euro 495 (Sh965,250).
Katika akaunti ya Benki ya NMB anamiliki Sh800,000 wakati katika Benki ya
Stanbic anamiliki akaunti ya familia yenye Dola za Marekani 1,000 (1.85
milioni) akiwa na asilimia 40 na dada yake Thabitha Salumu. Mbali na fedha,
Zitto anamiliki gari aina Rand Rover Freelander yenye thamani ya Dola za
Marekani 40,000 (Sh74 milioni).
Akizungumzia nyumba alizonazo, Zitto alisema moja ina
thamani ya Sh180 milioni na nyingine Sh43 milioni zote zikiwa mkoani Kigoma. (mwananchi.co.tz)
إرسال تعليق