JK AMLILIA MBITA ATOA WASIFU NADRA WATANZANIA KUUJUA

THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512, 2116898
Website : www.ikulu.go.tz              

Fax: 255-22-2113425

PRESIDENT’S OFFICE,
      STATE HOUSE,
              1 BARACK OBAMA ROAD,  
11400 DAR ES SALAAM.
Tanzania.
 
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho amepokea kwa majonzi na simanzi kubwa taarifa za kifo cha mmoja wa watumishi wa miaka mingi wa Serikali, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (TPDF), Chama cha TANU na Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Africa – Liberation Committee of the African National Unity (OAU), Brigedia Hashim Mbita, kiongozi ambaye Rais Kikwete amemwelezea kama mmoja wa viongozi ambao wameifanyia nchi yetu mengi na kwa miaka mingi.
Rais Kikwete ambaye amepokea taarifa za msiba huo mara ulipotokea asubuhi ya leo, Jumapili, Aprili 26, 2015 wakati alipoingia tu Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, kuongoza maelfu kwa maelfu ya wananchi kuadhimisha miaka 51 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ameuelezea msiba huo kama msiba wa simanzi kubwa.
“Ni wachache katika nchi yetu wanaoweza kulinganishwa na Mzee Hashim Mbita kwa kiwango cha utumishi uliotukuka, wa miaka mingi na usiokuwa na kasoro. Katika utumishi wa Serikali alipata kuwa Mwandishi wa Habari Mkuu wa Idara ya Habari na pia kuwa Mwandishi wa Habari wa Rais kabla na baadaye kuwa Balozi wa Tanzania katika Zimbabwe. Kazi zote alizifanya kwa ufanisi mkubwa sana,”amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Katika Chama cha TANU alikuwa Katibu Mtendaji wa Chama na katika Jeshi letu makini, Mzee Mbita alipata na kufikia cheo cha Brigedia Jenerali, yote mambo makubwa kweli kweli.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Lakini ilikuwa katika nafasi ya Katibu Mtendaji wa Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Afrika ambako Mzee Mbita alikamilisha utumishi wake kwa kusimamia shughuli nzito ya kuwasaidia ndugu zetu Kusini mwa Afrika kwa miaka 20 mfululizo, miongo miwili, na kuweza kupata uhuru wao. Hakuna mpigania uhuru katika Mozambique, katika Zimbabwe, katika Namibia, katika Angola na hatimaye katika Afrika Kusini ukiondoa nchi nyingine kama Cape Verde, asiyejua mchango wa Mzee Mbita. Wote hawa amewatumia vizuri, kwa ufanisi, kama mlezi, kama kiongozi, kama kamanda hadi wakafanikisha kazi ya ukombozi. Huu ni mchango mkubwa kweli kweli.”
Ameongeza Rais: “Kitendo chake cha mwisho cha utumishi, kilikuwa kuongoza shughuli za Mradi wa Hashim Mbita wa Kuweka Kumbukumbu za Harakati za Ukombozi Kusini mwa Afrika na Kuenzi Viongozi Wakuu (Hashim Mbita Project to Honour Outstanding Leaders), kazi ambayo nayo aliifanya kwa uwezo na ufanisi mkubwa na ripoti yake tukaizindua mwaka jana pale Victoria Falls, Zimbabwe wakati wa Mkutano wa Mwaka wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).”
Ilikuwa kwenye Mkutano huo wakati Zimbabwe ilitangaza kumpa Mzee Mbita Nishani ya The Royal Order Munhumutapa yenye kutambua mchango wake katika harakati za ukombozi wa Zimbabwe. Mzee Mbita amekuwa raia wa sita wa kigeni, na wa kwanza asiyekuwa rais, kupata heshima hiyo ya juu kabisa ambayo hutolewa na Taifa la Zimbabwe kwa wageni ambao wamechangia Uhuru wa Zimbabwe.
Viongozi watano wa mwanzo kupata Nishani hiyo, mwaka 2005, walikuwa ni Marais na Viongozi Waanzilishi wa Kundi la Nchi za Frontline States dhidi ya Ukoloni na Ubaguzi wa Rangi, Marehemu Julius Kambarage Nyerere, Mzee Kenneth David Kaunda wa Zambia, Marehemu Sir Seretse Khama wa Botswana, Marehemu Samora Moises Machel wa Mozambique na Marehemu Augustinho Neto wa Angola,
Ameongeza Rais Kikwete: “Mzee Mbita ametibiwa ndani na nje ya nchi na kila alipolazwa hapa nchini nilikwenda kumwona hospitali. Majuzi tu nilikwenda kumwona kwenye Hospitali ya Jeshi letu pale Lugalo na tukazungumza vizuri sikujua itakuwa mara yangu ya mwisho kuzungumza naye. Naungana na familia ya Mzee Mbita katika kuomboleza kifo na msiba wa Mzee wetu huyu. Nawaomba watambue kuwa msiba wa Mzee Mbita ni msiba wetu sote, msiba wa taifa letu ambalo limepoteza busara yake wakati tulipokuwa tunahitaji zaidi.”
Ameongeza Rais: “Tayari nimeagiza Serikali na Jeshi washirikiane na familia ya Mzee Mbita katika kuandaa matanga na mazishi ya Mzee wetu huyu. Wakati tunaendelea na maandalizi, nawaomba wanafamilia wawe na utulivu na subira kwa kadri tunapopitia kipindi hiki kigumu na kwa pamoja tuendelee kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehma kuiweka peponi roho ya Mzee Hashim Mbita. Amin.”
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
26 Aprili, 2015

Post a Comment

أحدث أقدم