JK amtunuku Koplo wa JWTZ aliyepambana na majambazi

Dar es Salaam. Koplo Laura Mushi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ni miongoni mwa Watanzania 42 waliotunukiwa nishani na Rais Jakaya Kikwete, Ikulu juzi Dar es Salaam.
Laura alitunukiwa Nishani ya Ushupavu ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 51 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Katika hafla hiyo Rais Kikwete alitunuku Nishani ya Kumbukumbu ya miaka 50 ya Muungano Daraja la Pili, la Tatu na la Nne, Nishani ya Muungano Daraja la Pili na Nishani ya Ushupavu.
Kabla ya kupokea nishani hiyo, ilielezwa kwamba usiku wa Machi 14 mwaka huu, Koplo Laura (32), akiwa kwenye kituo chake cha ulinzi, alivamiwa na kundi la majambazi waliomkaba kwa kamba na kumburuza kwa lengo la kutaka kumuua na kupora bunduki aliyokuwa nayo ikiwa na risasi 30.
Ilielezwa kwamba wakati majambazi hao wakimburuza kutoka katika lindo lake, Koplo Laura alijitahidi na kufanikiwa kudhibiti kamba hiyo isimnyime pumzi kwa kuwa walikwisha mfunga shingoni, huku akipambana kuzuia asinyang’anywe bunduki aliyokuwa nayo na kufanikiwa.
Alifanikiwa kuidhibiti kamba hiyo na kisha kuifikia chemba ya risasi ya bunduki na kuweza kufyatua risasi nne huku akiburuzwa.
Hali hiyo iliwafanya majambazi hao kumwachia na kukimbia, hivyo kuokoa maisha yake na silaha aliyokuwa nayo.
“Kitendo hicho kimeonyesha ushupavu, uzalendo na heshima ya hali ya juu kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania na wanawake wote nchini,” alisema mshereheshaji wa shughuli hiyo.
Akizungumza baada kupokea tuzo hiyo, Koplo Laura alisema: “Sikutarajia kupata nishani hii, imenitia moyo, nguvu na morali zaidi wa kufanya kazi kuilinda nchi yangu, pia kuonyesha kwamba inawezekana kila palipo na juhudi. Ninamshukuru Rais Jakaya Kikwete kwa kutambua mchango wangu.”
Katika hafla hiyo, watu wengine wa kada mbalimbali wakiwamo wanasiasa, watumishi wa umma pia wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama wastaafu na majaji wastaafu walitunukiwa nishani.
Kupitia nishani hizo, Rais Kikwete pia amemkumbuka marehemu Brigedia Jenerali Moses Nnauye aliyekuwa Katibu wa Oganaizesheni wa CCM na mwasisi wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), aliyetunukiwa Nishani ya Kumbukumbu ya Muungano Daraja la Tatu.
Nnauye alitajwa kushika nyadhifa mbalimbali ikiwamo kuongoza tume iliyoratibu kuunganishwa kwa vyama vya Tanu na ASP vilivyoungana mwaka 1977 na kuzaliwa CCM, huku mjane wa marehemu, Mwanaisha Nnauye aliyepokea nishani hiyo kwa niaba ya mumewe, akisema kuwa inamkumbusha jinsi Nnauye alivyokuwa mfanyakazi hodari na kipenzi cha watu kwa kujitolea kwake.

Post a Comment

أحدث أقدم