Kavumbagu awapa Yanga siku 30

Mshambuliaji wa kimataifa wa Azam, Mrundi, Didier Kavumbagu.

ISHU ya usajili wa mshambuliaji wa kimataifa wa Azam, Mrundi, Didier Kavumbagu, imechukua sura mpya baada ya kutoa kipindi cha muda wa mwezi mmoja ambapo ni sawa na siku 30, kabla hajajua kama atajiunga na Yanga ama la.
Kavumbagu ambaye amekuwa lulu katika kikosi cha Azam tangu atue msimu huu klabuni hapo akitokea Yanga, amekuwa akihusishwa mara kwa mara kurejea Jangwani, huku ikidaiwa kuwa tayari kuna mazungumzo ya siri kubwa yameanza baina yake na vigogo wa Yanga lakini yeye akasisitiza kutoa mwezi mmoja kabla ya kutangaza ameamua anakwenda wapi kwa ajili ya msimu ujao.
Mpaka sasa Kavumbagu amebakiza takriban miezi miwili ili kumaliza mkataba wake na Azam FC ambayo ilimsajili na kumpa mkataba wa mwaka mmoja.Kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), mchezaji huyo kwa sasa anaruhusiwa kufanya mazungumzo na timu nyingine yoyote.
Akizungumza na Championi Jumatano, Kavumbagu alifunguka kuwa hilo suala la kutakiwa na Yanga amekuwa akilisikia lakini kwa sasa hawezi kulitolea sana ufafanuzi kwa kuwa bado anaendelea kutafakari na kisha baada ya kipindi cha mwezi mmoja kupita, atakuwa tayari ameshajua muelekeo wake na kila mmoja atafahamu kuwa atakuwa wapi msimu ujao.
Aidha, Kavumbagu aliyefunga mabao 10 mpaka sasa kwenye ligi akizidiwa moja na kinara Simon Msuva wa Yanga mwenye 11, ameongeza kuwa anaamini kipindi cha mwezi mmoja kinamtosha zaidi kuisaidia Azam katika kuubakiza ubingwa Chamazi kisha baada ya hapo na yeye ndiyo atageukia upande wa pili na kuangalia zaidi maslahi yake.
“Kwa sasa siwezi kuwa na jibu la moja kwa moja kuhusiana na Yanga au Azam kwa sababu bado kuna muda zaidi hapa katikati na baada ya mwezi mmoja nitakuwa tayari nimeshapata jibu kichwani kama nitabaki Azam au nitakwenda Yanga au sehemu nyingine.
“Kwa sasa nataka kutoa sana msaada kwa timu yangu ya Azam kuhakikisha tunautetea ubingwa msimu huu na kipindi cha mwezi mmoja kinatosha kabisa kufanya hivyo.
“Kwa sababu baada ya mwezi zitakuwa zimebaki kama mechi mbili kumalizika kwa ligi na kama ni nani anatwaa ubingwa itakuwa tayari imeanza kubainika, kwa hiyo na mimi sasa hapo naweza kuangalia mambo yangu ya msimu ujao kuona itakuwaje, niamini nachokwambia kwamba baada ya muda huo kila kitu kitakuwa wazi na hakutakuwa na maswali mengine tena,”  alisema Kavumbagu.
Pamoja na hayo lakini Yanga inaonekana kuwa na asilimia nyingi zaidi za kumrejesha mchezaji wao huyo waliyemsajili kwa mara ya kwanza msimu wa 2012/13 akitokea Atletico ya Burundi baada ya kocha wa timu hiyo, Hans van Der Pluijm, kukiri kuwa ‘target’ zake katika usajili huu ni kupata straika mwenye vigezo kama alivyonavyo Kavumbagu kwa ajili ya kukisaidia kikosi chake kwenye mapambano ya msimu ujao.
Hata hivyo, mbali na hayo, mashabiki wa Yanga pia wameonyesha hali ya kuhitaji huduma ya straika wao huyo baada ya kumueleza wazi kumtaka arudi nyumbani walipokutana naye jijini Tanga, Yanga ilipokuwa ikiumana na Mgambo Shooting na Azam ilipokwenda kucheza na Coastal Union.
Kwa upande mwingine Azam leo itapata pigo kwa kumkosa mshambuliaji wake huyo katika mchezo wao dhidi ya Mbeya City utakaopigwa kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar kutokana na kuwa na kadi tatu za njano.

Post a Comment

Previous Post Next Post