Moshi. Meya wa Mji wa Moshi, Jaffar Michael amesema kufungwa kwa
Soko Kuu la Kati mjini Moshi na kufunguliwa kwa amri ya Katibu Mkuu wa
CCM, Abdulrahman Kinana ni sinema ya kisiasa.
Hivi karibuni Kinana alipokuwa katika ziara mjini
hapa, alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, kuhakikisha
soko hilo hadi kufikia Aprili 9 mwaka huu, liwe limefunguliwa.
Soko hilo lilifungwa Aprili mwaka jana kwa amri ya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kutokana na kutokidhi vigezo vya usafi.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara juzi kwenye
uwanja wa Soko la Pasua, Meya Michael alidai kufungwa kwa soko hilo ni
mchezo wa kisiasa.
“Inaonekana ni mkakati ulipangwa kwamba soko lile
lifungwe ili itengenezwe chuki kati ya Chadema na wananchi wake. Baada
ya muda lifunguliwe,” alisema Meya Michael.
Aliwashauri wafanyabiashara walioathirika kutokana na kufungwa kwa soko hilo wadai fidia na kama wasipolipwa waende mahakamani.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Manispaa ya
Moshi, Priscus Tarimo alikanusha kuwapo kwa mchezo wowote wa kisiasa,
akisema chama kiliangalia masilahi ya wafanyabiashara.
“Serikali iliyopo madarakani ni ya CCM kwa hiyo
Kinana aliagiza Serikali kwamba soko lifunguliwe wakati fedha za
kukarabati zinatafutwa. Wafanyabiashara wameteseka kwa mwaka mzima,”
alisema.
Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo
alipoulizwa kuhusu sakata hilo alisema jambo hilo ni zito na atalitolea
msimamo katika mkutano wa hadhara utakaofanyika leo kwenye viwanja vya
Manyema.

Post a Comment