VPL KUENDELEA KESHO
Ligi
Kuu ya Vodacom Tanzania inatarajiwa kuendelea kesho jumatano katika
viwanja viwili nchini, jijini Tanga wenyeji Maafande wa Mgambo Shooting
watawakaribisha timu ya Azam FC kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
Mjini
Morogoro wakata miwa wa Mtibwa Sugar watakua wenyeji wa maafande wa
jeshi la Magereza nchini timu ya Tanzania Prisons kutoka Mbeya, mchezo
utakaopigwa katika dimba la Manungu Turiani.
KAMATI YA MASHINDANO TFF
Kamati
ya Mashindano ya TFF ilikutana jana kupitia maandalizi ya Ligi ya
Mabingwa wa Mikoa (RCL) pamoja na taarifa ya Ligi Daraja la Pili (SDL)
iliyomalizika hivi karibuni.
Katika
matukio ya SDL, Kamati imeipiga faini ya sh. 300,000 timu ya JKT
Rwamkoma ya Mara kwa kusababisha mechi yake dhidi ya AFC ya Arusha
kuvurugika. Adhabu hiyo kwa mechi hiyo iliyofanyika Uwanja wa Kumbukumbu
ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha imetolewa kwa kuzingatia
Kanuni ya 28(4) ya Ligi Daraja la Pili.
Nao
makocha wa JKT Rwamkoma, Hassan Makame na Kamara Kadede wamepigwa faini
ya sh. 200,000 kila mmoja na kufungiwa mechi sita kwa kumshambulia
mwamuzi msaidizi namba moja katika mechi hiyo iliyochezwa Machi 9, 2015.
Wachezaji
Shafii Maganga, Saleh Ali, Ismail Salim na Mussa Senyange wa JKT
Rwamkoma ambao wanatuhumiwa kwa kushambulia mwamuzi kwenye mechi hiyo
suala lao linapelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa hatua zaidi.
TFF YAFUNGUA SEMINA YA WAAMUZI VIJANA
Katibu
Mkuu wa TFF Mwesigwa Selestine leo amefungua rasmi semina ya waamuzi
vijana wenye umri wa miaka 12- 17, inayofanyika katika hostel za TFF
zilizopo Karume.
Akiongea
na waandishi wa habari, Mwesigwa amesema semina hiyo ya vijana
imejumuisha vijana 27 kutoka mikoa mbalimbali nchini kwa lengo la
kuwaandaa kuwa waamuzi wa kimataifa baadae.
Vijana
hawa mnaowaona hapa wanatoka katika viuto vya kufundishia waamuzi
vijana nchini, wakikua na kufuata misingi ya kazi baadae watakua waamuzi
bor nchini kwa sababu watakua wameanza tangu wadogo na kufuata
maelekezo ya wakufunzi wao.
Naye
Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi nchin Bw. Salum Chama akiongea na
wandishi wa habari kabla ya kumkaribisha katibu mkuu, amesema malengo
yao ni kuhakikisha Tanzania inakuwa na waamuzi wa kimataifa wengi.
Mwaka
huu Tanzania imeshika nafasi ya pili kwa kutoa waamuzi 18 wenye beji za
FIFA barani Afrika, nyuma ya Misri yenye waamuzi 22, Lengo ni
kuhakikisha tunawaanda vijana wengi waje kuwa waamuzi wa kimataifa.
Semina
hiyo ya siku 5 inatarajiwa kufungwa ijumaa tarehe 17 Mei, 2015
inajumuisha vijana kutoka mikoa ya Dar es salaam, Tanga, Zanzibar,
Mwanza, Arusha na Mbeya, kati ya vijana 37 waamuzi wawili ni wanawake.
Wakufunzi wa semina hiyo ni Soud Abdi, Riziki Majala na Joan Minja.
KAMATI YA USIMAMIZI NA UENDESHAJI YA BODI YA LIGI
Kocha
Jackson Mayanja wa Kagera Sugar amepigwa faini ya sh. 500,000 na
kufungiwa mechi tatu kwa kutoa lugha ya kashfa kwa maneno na vitendo kwa
waamuzi wa mechi yao na Mtibwa Sugar kuwa walipewa rushwa.
Adhabu
dhidi ya Kocha Mayanja kwenye mechi hiyo namba 136 iliyochezwa Aprili
1, 2015 kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga imetolewa kwa
kuzingatia kanuni ya 40(1) ya Ligi Kuu.
Klabu
ya Mtibwa Sugar imepigwa faini ya sh. 500,000 baada ya timu yake
kukataa kuingia vyumbani wakati wa mapumziko katika mechi namba 142
dhidi ya Stand United iliyochezwa Aprili 5, 2015 katika Uwanja wa
Kambarage mjini Shinyanga. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa kanuni
ya 14(13) ya Ligi Kuu.
Nayo
Simba imepigwa faini ya sh. 300,000 kwa mujibu wa kanuni ya 14(9) ya
Ligi Kuu baada ya timu yao kugoma kuingia kwenye vyumba vya kuvalia nguo
(changing room) kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga wakati wa
mechi dhidi ya Kagera Sugar. Hatua hiyo ilisababisha wachezaji
wakaguliwe kwenye gari lao.
Pia
Simba imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kuzingatia kanuni ya 14(13) ya
Ligi Kuu baada ya vilevile kugoma kuingia vyumbani wakati wa mapumziko
kwenye mechi hiyo hiyo namba 146 iliyochezwa Aprili 6, 2015.
Kipa
Tony Kavishe wa Polisi Morogoro amepigwa faini ya sh. 500,000 na
kufungiwa mechi tatu kwa kosa la kumpiga ngumi mwamuzi msaidizi namba
mbili, Hassan Zani kwa kuzingatia kanuni ya 37(5) ya Ligi Kuu. Alifanya
kosa hilo kwenye mechi namba 147 dhidi ya Mgambo Shooting iliyochezwa
Aprili 5, 2015 katika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Post a Comment