NIANZE kwa kumshukuru Mungu wa Mbinguni kwa kunikutanisha na wewe msomaji wangu katika safu hii ya Show The Love. Huu ndiyo uwanja pekee ambao tunaweza kupashana masuala mbalimbali yahusuyo mapenzi.
Niwashukuru wale wote mnaotuma maoni yenu kuashiria mnaguswa na mada ambazo tumekuwa tukizijadili katika safu hii kila Jumamosi. Cha msingi ni kujifunza na kuyafanyia kazi yale yote ambayo tumekuwa tukiyajadili ili kudumisha maisha yetu ya uhusiano.Kwa moyo mkunjufu nikukaribishe katika mada ya leo ambayo kichwa cha habari kinajieleza hapo juu. Kwenye maisha, vipo vitu vingi sana wanandoa wanashirikiana lakini lipokuja suala la kipato huwa kila mtu anakuwa na mtazamo wake kulingana na sababu zake anazoziamini mwenyewe.
Kuna baadhi ya wanaume ambao wameoa huwa wanaamini kwamba, mke hawapaswi kujua kipato chao. Mke hapaswi kuhoji mshahara anaoupata mumewe kwa mwezi. Anachotakiwa yeye ni kusema tu kitu flani kimeisha, kipi kimepungua ili mwanaume atoe fedha yeye akanunue kama ana fedha na kama hana basi atamwambia asubiri siku akipata ampatie.
Wanaume hao huwa wanaamini kwamba, mwanamke unapomueleza kipato chako chote cha mwezi ni dhahiri kwamba atakuwa msumbufu.Wanaamini mkewe atakuwa anafuja fedha katika matumizi ya kila siku akiamini mumewe anamudu kwani anatambua mshahara wote wa mumewe.
Ili kuepusha maswali ya ‘baba fulani mshahara wote umekwenda wapi?’ ndipo anapoona bora amfiche mke wake. Hata kama ikitokea amemwambia basi anamficha kidogo ili aweze kubaki na salio pembeni la kufanyia shughuli zake binafsi ikiwemo unywaji wa pombe kama anatumia au mambo mengine yanayofanana na hilo.
Wanaume wa aina hiyo huwa wanaona mshahara ni mali yake. Mke hapaswi kujua, suala la msingi yeye atoe bajeti yake ya mwezi mzima, apewe fedha hizo na si kuhoji pato zima analolipata mwenzake kwa mwezi mzima, iwe ni kazi ya kuajiriwa au ya kujiajiri. Kuna mfano mmoja wa mwanaume ambaye yupo ndani ya ndoa kwa zaidi ya miaka 7 niliwahi kuzungumza naye, akaniambia yeye kamwe hawezi kumwambia mkewe mshahara wake ili asimbane katika starehe zake:
“Binafsi kamwe siwezi kumueleza kipato changu mke wangu hata siku moja maana ukimwambia tu itakuwa shida.
Atataka bajeti yote apange yeye, wewe kazi yako itakuwa ni kupokea mshahara na kuukabidhi kwake sasa itakuwa na maana gani mimi niwe nafanya kazi halafu hata nikitaka kuchangamsha akili na bia moja au mbili nimuombe tena yeye, itakuwa haina maana hata mimi kufanya kazi sasa.”
Hapo ndipo utagundua kwamba aina ya wanaume hao ni wale wanaoamini kuwaambia wake zao juu ya suala la kipato chao kutawakoseshea starehe zao binafsi. Wanahofia kutawaliwa, wanaona ni vyema kuficha kipato chao ili starehe nyingine wazifanye bila wake zao kujua kinachoendelea.
Si wanaume peke yao, wapo pia wanawake ambao nao pato lake huwa linabaki kuwa la kwake lakini la mume linakuwa la wote. Kamwe hawezi kumueleza mumewe kuwa anaingiza shilingi ngapi kwa siku au kwa mwezi katika biashara yake au katika kazi aliyoajiriwa.
Kama ilivyokuwa kwa wanaume, wanawake hao nao wanaamini kuwa, wakiwaeleza waume zao kipato chao wanaume watataka kuwatawala. Wanaamua kuwaficha ili waweze kutumbua fedha zao kimyakimya.
Itaendelea wiki ijayo.
إرسال تعليق