Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limemtaka Mkuu wa
Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima, kuhamisha makazi ya
kanisa lake lililopo katika viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe,
jijini Dar es Salaam leo.
Meneja Uhusiano wa NHC, Yahya Charahani alilieleza NIPASHE kuwa,
walimpatia notisi Askofu Gwajima ya kuhama eneo hilo mwezi mmoja
uliopita, lakini hakutekeleza badala yake ameendelea kulitumia eneo hilo
kuendesha shughuli za kanisa lake, zikiwamo ibada.
Charahani alisema eneo hilo ni mali ya NHC na ni maalum kwa ajili
ya ujenzi wa mji wa kisasa na wakazi waliokuwa wanaoishi eneo hilo
walishalipwa fidia muda mrefu uliopita ili kuondoka.
“Lile eneo ni la NHC kwa muda mrefu na kabla ya hapo kulikuwa na
nyumba nyingi sana na zilibomolewa, hizo zilizobaki zimebaki tu
kimakosa,” alisema Charahani.
Aliongeza kuwa, hiyo siyo mara ya kwanza kwa NHC kumpatia notisi Askofu kiongozi huyo kulihamisha kanisa lake.
Kwa mujibu wa Charahani, NHC walimpatia notisi Askofu Gwajima ya
mwezi mmoja kuondoka katika makazi hayo na kwamba notisi hiyo
ilimalizika Machi 9, mwaka huu.
Alisema baada ya kumalizika kwa notisi hiyo, NHC lilimpatia muda zaidi Askofu huyo ambao unamalizika leo.
Juhusi za kumpata Askofu Gwajima kuthibitisha kama amepokea notisi
hiyo zilishindikana kutoka na simu yake ya mkononi kutopatikana kila
alipopigiwa tangu Alhamisi iliyopita.
Hata hivyo, jana alipotafutwa Mwanasheria wa Askofu Gwajima, Paul
Mallya kuelezea hatua ya NHC ya kumpa mteja wake notisi ya kuhamisha
makao ya kanisa lake, alisema bado hajapata notisi hiyo.
“Sijapata taarifa hiyo, ndiyo kwanza nasikia kwako, ngoja nifuatilie nije nikupe majibu yaliyokamilika,” alisema Mallya.
Post a Comment