Mbeya. Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Nyerembe Sabi, amempigia debe
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira, pale alipoeleza
kuwa yeye siyo waziri na mbunge tu, bali ni mtarajiwa.
Alisema hayo katika mkutano wake na Watafiti wa Taasisi ya Maendeleo na Utafiti wa Mazao Uyole, uliofanyika mwishoni mwa juma.
Mkuu huyo wa wilaya alitoa kauli hiyo alipokuwa
akimkaribisha Waziri Wasira kwenye hafla ya kufunga utafiti wa mbegu
bora za viazi mvirigno, uliokuwa ukifanywa na taasisi ya Ari Uyole kwa
udhamini wa Nchi ya Ufini (Finland)
Utafiti huo ulianza 2011 na ulimalizika mwishoni
mwa juma na wakulima wataanza kutumia mbegu hizo bora katika msimu huu
wa kilimo. Mbegu hizo zinatoa tani 18 kwa ekari badala ya tani tano au
nane za awali.
“Mheshimiwa Waziri, mbunge ambaye pia ni
mtarajiwa’’ alisema mkuu huyo wa wilaya bila kumalizia ni mtarajiwa wa
nini na kusababisha watu kuangua kicheko.
Ingawa mkuu huyo wa wilaya hakutaka kusema Wasira
anatarajia nini, tayari mbunge huyo wa Bunda amewaambia baadhi ya
wanaCCM kuwa anatarajia kugombea urais katika uchaguzi mkuu ujao.
Nia hiyo ya Wasira kuutaka urais, inathibitishwa
pia na uamuzi wa CCM kumwadhibu kwa kuanza kampeni mapema, sambamba na
makada wengine watano wa chama hicho, akiwamo Bernard Membe, Frederick
Sumaye, Edward Lowassa, Januari Makamba na William Ngeleja.
Alipoulizwa na mwandishi kwa nini anaitwa mtarajiwa, Wasira alijibu kwa kifupi, “ Kamuulize DC mwenyewe atakueleza”.
Katika hotuba na mazungumzo yake kwenye hafla
hiyo, Wasira hakugusia suala la uchaguzi ama urais bali alijikita zaidi
kwenye umuhimu wa suala la utafiti wa mbegu bora kwa manufaa ya
wakulima.
Pia Wasira aliwalaumu maofisa kilimo nchini,
akisema wameshindwa kazi waliyotumwa na Serikali ya kwenda kubadili
maisha ya wananchi wa vijijini kwa kuwaongoza katika kilimo chenye tija
Post a Comment