Dar es Salaam. Wakati mashambulizi ya kigaidi
yakiendelea kutikisa maeneo mbalimbali duniani ikiwamo nchi jirani ya
Kenya huku kukiwa na angalizo kuwa huenda na Tanzania ikashambuliwa,
jarida moja la kimataifa limetaja mambo 10 ya kufanya baada ya
shambulio.
Mambo hayo ambayo ni hatua za kumsaidia mtu
aliyenusurika katika shambulio husika ili kunusuru maisha yake,
yametajwa wakati zikiwapo taarifa za tisho la shambulizi katika miji ya
Dar es Salaam na Mwanza.
Jarida hilo lilifanya mahojiano na wataalamu wa
sayansi ambao walitoa mapendekezo ambayo mtu anaweza kufuata wakati au
baada ya mlipuko na kuwa asilimia 50 ya watu wanaokutwa katika
mashambulizi ya kigaidi hujeruhiwa na wengine kupoteza maisha kwa
sababu hawafahamu jinsi ya kujihami.
Tanzania iliwahi kukumbwa na shambulio la ugaidi
mwaka 1998 wakati Ubalozi za Marekani, jijini Dar es Salaam
ulipolipuliwa na kusababisha vifo vya watu kumi na moja. Shambulio hilo
lilitokea sambamba na lile la ubalozi wa nchi hiyo, Nairobi, Kenya
lililosababisha vifo ya watu 213.
Uvumi zaidi umeendelea kuenea baada ya shambulio
la kigaidi lililotokea wiki iliyopita katika Chuo Kikuu cha Garissa,
Kenya na kuua wanafunzi 148.
Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Mathias Chikawe alisema pamoja na kusikia taarifa hizo, mpaka sasa
Serikali haijaweza kuthibitisha ripoti hizo zinazoenea, lakini inachukua
tahadhari juu ya suala hilo.
Polisi, Serikali wajiandaa
Akizungumzia tahadhari mbalimbali za mashambulizi
ya kigaidi au Watanzania kushiriki katika ugaidi, Kaimu Mkurugenzi wa
Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Diwani Athuman alisema hali hiyo ina
taswira kuwa Taifa si salama kwa asilimia 100.
“Kuna usemi usemao mwenzako akinyolewa wewe tia
maji, Tanzania si kisiwa, kuna changamoto kubwa kwa sababu tumepakana na
wenzetu Kenya ambao wameathiriwa na ugaidi, ndiyo maana hatuwezi kusema
tupo salama kwa asilimia 100,” alisema.
Alisema kutokana na hali ilivyo sasa, Watanzania
hawana budi kutilia mkazo umoja kama njia ya kutokomeza uhalifu na
kuacha kushabikia masuala ya ugaidi.
Kuhusu vijana kujiunga na makundi ya ugaidi,
Diwani alisema wazazi hawana budi kuwafuatilia watoto huko shuleni ili
wajue kinachoendelea.
“Tanzania ni lazima irudi kule ambako ilikuwa.
Kila mmoja ni mlinzi wa mwingine, sasa hivi watoto wanaachwa hadi
wanapumbazika na kujiunga na makundi ya ugaidi. Hii si kazi ya vyombo
vya dola peke yake ni ya kila mmoja,” alisema
إرسال تعليق