Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda amemwandikia barua Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima akimtaka afike mbele ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya kwa mahojiano.
Inaelezwa kuwa Makonda alimtumia Askofu Gwajima barua hiyo Machi 30 mwaka huu, akiwa amelazwa katika Hospitali ya TMJ.
Hata
hivyo, kiongozi huyo wa kiroho amegoma akisema hawezikwenda ofisini kwa
mkuu huyo wa wilaya kwa mahojiano. Mmoja wa wasaidizi wa Askofu Gwajima
alisema jana kuwa hatua ya Makonda kumtumia barua haikumpendeza
kiongozi huyo wa kanisa.
“Makonda
alikuja katika Hospitali ya TMJ na kudai amekuja kumwona Askofu Gwajima
huku akiwa amebeba barua yake. Baada ya kumwuliza hali ya maendeleo ya
afya yake alitoa barua na kumkabidhi jambo ambalo halikuwa jema.
“Baada
ya muda Askofu Gwajima alituita wasaidizi wake na kutueleza kuwa
amepewa barua ya wito kwa DC, sasa tukajiuliza askofu anaumwa. Je,
inakuaje aende tena katika mahojiano na mkuu wa wilaya? “Na kama ni
hivyo nini kazi ya polisi maana wamemuhoji tangu siku ya kwanza baada ya
kumkamata.
Mtu
anahojiwa na polisi sasa inakuaje tena aitwe na DC ahojiwe na kamati ya
ulinzi? Amesema hatokwenda,” alisema msaidizi huyo wa Gwajima ambaye
hakutaka jina lake litajwe.
Mkuu
wa Wilaya ya Kinondoni Paul Makonda alitoa ufafanuzi wa barua yake
hiyo, ambapo alijibu kwa kifupi kuwa ni kweli amemwandikia barua ya wito
kiongozi huyo. Alipoulizwa ni hatua zipi Askofu Gwajima atachukuliwa
kwa kutaa kutii wito huo, Makonda alisema.“Kuhusu hatua subirini mtaziona wenyewe” alisema mkuu huyo wa wilaya.
Gwajima
kuripoti polisi Wakati hohuo, Askofu Gwajima leo anatarajiwa kuripoti
katika Kituo Kuu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kuendelea
kuhojiwa kuhusiana na tuhuma zinazomkabili.
Gwajima
aliachiwa kwa dhamana juzi baada ya kutoka katika Hospitali ya TMJ
ambako alikuwa amelazwa kwa matibabu baada ya kuanguka ghafla wakati
akihojiwa na polisi.
Mwanasheria wa Gwajima, John Mallya alisema baada ya kuruhusiwa juzi, leo anatakiwa kuripoti tena katika kituo hicho kuendelea na mahojiano. “Polisi
walituambia twende kesho (leo) kwa mahojiano kwa sababu yalikuwa
hayajakamilika… lakini tunaamini polisi wanaweza kumruhusu kurudi
nyumbani kupumzika au kuendelea na mahojiano mengine,” Mallya.
Alisema
mpaka sasa anaendelea vizuri na matibabu na afya yake inaendelea
kuimarika siku hadi siku tofauti na alivyokuwa awali. Gwajima
alifikishwa polisi kwa madai ya kumtukana na kumkashifu Askofu Mkuu wa
Kanisa Katoliki Jimbo la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.
Wakati
anahojiwa alianguka na kuzimia hali iliyosababisha akimbizwe katika
hospitali ya polisi Kurasini kabla ya kuhamishiwa katika Hospitali ya
Taifa Muhimbili (MNH) na baadaye Hospitali ya TMJ kwa matibabu zaidi.
Juzi Askofu Gwajima alikwenda polisi akiwa amepandishwa kwenye baiskeli maalumu ya wagonjwa.

إرسال تعليق