Dar es Salaam. Mtoto wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Yusufu
Makamba, Mwamvita Makamba amenusurika kifo nchini Afrika Kusini baada ya
kundi la watu wasiojulikana kuvamia gari lake na kumrushia risasi.
Mwamvita, ambaye anafanya kazi nchini humo
alikumbana na kadhia hiyo juzi usiku alipokuwa akisafiri kutoka
Johannesburg kuelekea Sun City kwa shughuli za kiofisi.
Akizungumzia tukio hilo jana kutoka Afrika Kusini,
Mwamvita alisema katika safari yake hiyo alifika sehemu ambayo alikuta
matairi yamechomwa na kuona kundi la watu jambo lililomfanya ageuze gari
haraka.
“Sehemu nyingi hapa Afrika Kusini wana vurugu sana
kama Serikali haijawatekelezea mahitaji yao, hivyo katika eneo hilo
ambalo nilikuta watu hao wakati napita niligundua kulikuwa na vurugu
nikageuza gari,”alisema na kuongeza:
“Wale watu wakaanza kurusha mawe na wakapiga
risasi ambayo ilivunja kioo cha gari langu na ilidondoka kwenye kiti cha
pembeni kwenye gari. Nashukuru Mungu haikunipata. Nikaendesha hadi
kituo cha polisi kutoa taarifa.”
Alisema tukio hilo halihusiani na kinachoendelea
sasa katika mji wa Durban kwa Waafrika Kusini kuwakimbiza na kuua wageni
bali ni jambo la kawaida nchini humo kutokea vurugu za mara kwa mara.
Post a Comment