Wazee wa CCM Hai wapania kumg'oa Mbowe .

Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe.
Baadhi ya wazee wa jimbo la Hai, mkoani Kilimanjaro, wamemwita jimboni humo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru, Danstan Malya, wakimtaka afanye uamuzi mgumu wa kurejea nyumbani, kumkabili Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, kinyang'anyiro cha ubunge Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
 
Malya ni miongoni mwa makada watatu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wanaotajwa kutaka kumng’oa Mbowe kwenye kiti chake cha ubunge kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba mwaka huu. Wengine ni Mbunge wa zamani, Fuya Kimbita na Katibu wa CCM Wilaya ya Monduli mkoani Arusha, Elisante Kimaro.
 
Uamuzi huo ulitangazwa jana na kiongozi wa wazee hao, Mathew Kimaro, kwenye mkutano na waandishi wa habari, Boma Ng’ombe.
 
“Kupitia tamko hili, tunamwomba mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Meru, Dastan Malya, arejee nyumbani ili ashiriki harakati za kulikomboa jimbo hili kutoka mikononi mwa chama kikuu cha upinzani nchini. Tunajua anao uwezo, ndiyo maana tunakwenda pia kumshawishi atangaze nia baada ya CCM kupuliza kipenga,” alisema.  
 
Kada wa chama hicho, Mustapha Hassan, mkazi wa Masama, alisema “Tunamshawishi agombee, kwa sababu tunaamini kwamba anao uwezo wa kulikomboa jimbo mikononi mwa Chadema, ambao wameliongoza kwa vipindi viwili vya mwaka 2000 hadi 2005 na baadae mwaka 2010 hadi sasa. Kama hakutakuwa na mizengwe ndani ya chama chetu, Mbowe ataanguka katika uchaguzi mkuu ujao,” alisema.
 
Wazee waliojitokeza kumfuata na kumshawishi Malya ni wa vijiji vya Mungushi, Sanya Station, Rundugai, Mnadani, Machame Kusini, MailiSita na Kalali.
 
Hata hivyo, Malya alipoulizwa na NIPASHE kuhusu hatua hiyo ya wakazi wa Wilaya ya Hai, alikiri kufuatwa na baadhi ya wazee wakimshawishi kutangaza nia ya kugombea ubunge katika jimbo hilo kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Uchaguzi Mkuu ujao. "Ni kweli walikuja wazee wa Hai, huku mkoani Arusha na kuniomba niende nikagombee, nikawaeleza kwamba natafakari lakini nikawaahidi kwamba wakati ukifika nitatangaza nia hiyo," alisema Malya

Post a Comment

Previous Post Next Post