Nyalandu amaliza mgogoro wa ardhi uliodumu miaka saba.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.
Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimempongeza Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu (pichani) , kwa kufanya uamuzi sahihi wa kumaliza mgogoro wa ardhi wilayani Mbarali uliodumu takriban miaka saba.
 
Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, Mathayo Mwangomo, ambaye alisema mgogoro huo umekuwa kikwazo cha maendeleo ya wananchi hao.
 
Alisema ulikuwa unaohusisha wananchi wa vijiji 21 ambao walitakiwa kuhama kwa madai ya kuingia kwenye eneo la Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.
 
Alisema awali wananchi walikubali kuachia sehemu ya ardhi kwa ajili ya hifadhi hiyo, lakini wataalamu waliohusika waliongeza eneo ambalo halikuwemo kwenye makubaliano na hapo ndipo mgogoro  ulipoibuka.
 
Alisema uamuzi wa Nyalandu kutangaza kufuatwa kwa taratibu na kuagiza wananchi hao kutohamishwa, umeleta amani na mshikamano.
 
“Tunakupongeza kwa dhati kabisa kwa kutatua mgogoro huu ambao ulionekana kama mfupa mgumu...wenzako wengi walishindwa kuutolea uamuzi, lakini kwa kuthibitisha wewe ni kiongozi makini na mtendaji wa kweli umemaliza kazi," alisema na kuongeza: “Hali ilikuwa tete miongoni mwa viongozi wa CCM na watendaji wengine kuhusiana na mgogoro huu...wapo waliotuhumiwa kuhongwa ili kuhakikisha wananchi wanahamishwa hivyo, kujenga chuki na sintofahamu huku wananchi wakiwa na hasira na Chama na serikali yao. Kwa sasa umeleta matumaini mapya na hilo limedhihirika na mapokeo na furaha waliyonayo wananchi wa Mbarali baada ya kuwatangazia,” alisema.
 
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara, Nyalandu alisema wananchi hao wataendelea  na maisha yao mahali walipo kwa sababu alishazungumza na Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye alimweleza hawatahamishwa.
 
Nyalandu alitumia fursa hiyo pia kuwataka wananchi kuheshimu mipaka ya hifadhi za jamii pamoja na kutoa ushirikiano kwa askari wa wanyamapori.
 
Aliwaeleza kuwa ni kosa kwa wananchi kuvamia ardhi zilizotengwa kwa ajili ya hifadhi na kwamba uamuzi huo haumaanishi maeneo mengi wavunje sheria wakiamini serikali itawaonea huruma.
 
Awali waziri  Nyalandu alikutana na kufanya kikao na uongozi wa CCM wakiwamo wajumbe wa halmashauri kuu, ambao walitoa maoni na chanzo cha mgogoro huo.
 
Kikao hicho kilitawaliwa na msuguano miongoni mwa wajumbe kwa kile kilichoelezwa awali na Mwangomo kuwa kuna chuki zimetanda miongoni mwa makada hao kuhusiana na mgogoro huo.
 
Baadhi ya wajumbe waliwatupia lawama viongozi kuwa wamegeuza mgogoro huo kama kitega uchumi kwa kuunda kamati mbalimbali, ambazo hazitoi suluhisho zaidi ya kulipwa posho. Shaban Sawasawa alisema mgogoro huo umewanufaisha baadhi ya watendaji na viongozi kwa muda mrefu na kuwa, hatua ya Nyalandu kuumaliza imedhihirisha uchakapazi wake na mapenzi mema aliyonayo kwa Watanzania.
 
“Kuna viongozi hatuna imani nao wakiwemo wasaidizi wako wizarani huko...tunashukuru umefika hapa na kutoa suluhisho bila kuunda kamati za kulipana posho kama ilivyokuwa kwa wengine,” alisema.

Post a Comment

Previous Post Next Post