Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimempongeza Waziri wa
Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu (pichani) , kwa kufanya uamuzi
sahihi wa kumaliza mgogoro wa ardhi wilayani Mbarali uliodumu takriban
miaka saba.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mbarali mkoani
Mbeya, Mathayo Mwangomo, ambaye alisema mgogoro huo umekuwa kikwazo cha
maendeleo ya wananchi hao.
Alisema ulikuwa unaohusisha wananchi wa vijiji 21 ambao walitakiwa
kuhama kwa madai ya kuingia kwenye eneo la Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.
Alisema awali wananchi walikubali kuachia sehemu ya ardhi kwa ajili
ya hifadhi hiyo, lakini wataalamu waliohusika waliongeza eneo ambalo
halikuwemo kwenye makubaliano na hapo ndipo mgogoro ulipoibuka.
Alisema uamuzi wa Nyalandu kutangaza kufuatwa kwa taratibu na kuagiza wananchi hao kutohamishwa, umeleta amani na mshikamano.
“Tunakupongeza kwa dhati kabisa kwa kutatua mgogoro huu ambao
ulionekana kama mfupa mgumu...wenzako wengi walishindwa kuutolea uamuzi,
lakini kwa kuthibitisha wewe ni kiongozi makini na mtendaji wa kweli
umemaliza kazi," alisema na kuongeza: “Hali ilikuwa tete miongoni mwa
viongozi wa CCM na watendaji wengine kuhusiana na mgogoro huu...wapo
waliotuhumiwa kuhongwa ili kuhakikisha wananchi wanahamishwa hivyo,
kujenga chuki na sintofahamu huku wananchi wakiwa na hasira na Chama na
serikali yao. Kwa sasa umeleta matumaini mapya na hilo limedhihirika na
mapokeo na furaha waliyonayo wananchi wa Mbarali baada ya kuwatangazia,”
alisema.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara, Nyalandu alisema wananchi
hao wataendelea na maisha yao mahali walipo kwa sababu alishazungumza
na Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye alimweleza hawatahamishwa.
Nyalandu alitumia fursa hiyo pia kuwataka wananchi kuheshimu mipaka
ya hifadhi za jamii pamoja na kutoa ushirikiano kwa askari wa
wanyamapori.
Aliwaeleza kuwa ni kosa kwa wananchi kuvamia ardhi zilizotengwa kwa
ajili ya hifadhi na kwamba uamuzi huo haumaanishi maeneo mengi wavunje
sheria wakiamini serikali itawaonea huruma.
Awali waziri Nyalandu alikutana na kufanya kikao na uongozi wa CCM
wakiwamo wajumbe wa halmashauri kuu, ambao walitoa maoni na chanzo cha
mgogoro huo.
Kikao hicho kilitawaliwa na msuguano miongoni mwa wajumbe kwa kile
kilichoelezwa awali na Mwangomo kuwa kuna chuki zimetanda miongoni mwa
makada hao kuhusiana na mgogoro huo.
Baadhi ya wajumbe waliwatupia lawama viongozi kuwa wamegeuza
mgogoro huo kama kitega uchumi kwa kuunda kamati mbalimbali, ambazo
hazitoi suluhisho zaidi ya kulipwa posho. Shaban Sawasawa alisema
mgogoro huo umewanufaisha baadhi ya watendaji na viongozi kwa muda mrefu
na kuwa, hatua ya Nyalandu kuumaliza imedhihirisha uchakapazi wake na
mapenzi mema aliyonayo kwa Watanzania.
“Kuna viongozi hatuna imani nao wakiwemo wasaidizi wako wizarani
huko...tunashukuru umefika hapa na kutoa suluhisho bila kuunda kamati za
kulipana posho kama ilivyokuwa kwa wengine,” alisema.
إرسال تعليق