Baadhi ya wazee wa jimbo la Hai, mkoani Kilimanjaro,
wamemwita jimboni humo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya
Meru, Danstan Malya, wakimtaka afanye uamuzi mgumu wa kurejea nyumbani,
kumkabili Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Freeman Mbowe, kinyang'anyiro cha ubunge Uchaguzi Mkuu wa
mwaka huu.
Malya ni miongoni mwa makada watatu wa Chama cha Mapinduzi (CCM),
wanaotajwa kutaka kumng’oa Mbowe kwenye kiti chake cha ubunge kwenye
Uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba mwaka huu. Wengine ni Mbunge wa zamani,
Fuya Kimbita na Katibu wa CCM Wilaya ya Monduli mkoani Arusha, Elisante
Kimaro.
Uamuzi huo ulitangazwa jana na kiongozi wa wazee hao, Mathew Kimaro, kwenye mkutano na waandishi wa habari, Boma Ng’ombe.
“Kupitia tamko hili, tunamwomba mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya
ya Meru, Dastan Malya, arejee nyumbani ili ashiriki harakati za
kulikomboa jimbo hili kutoka mikononi mwa chama kikuu cha upinzani
nchini. Tunajua anao uwezo, ndiyo maana tunakwenda pia kumshawishi
atangaze nia baada ya CCM kupuliza kipenga,” alisema.
Kada wa chama hicho, Mustapha Hassan, mkazi wa Masama, alisema
“Tunamshawishi agombee, kwa sababu tunaamini kwamba anao uwezo wa
kulikomboa jimbo mikononi mwa Chadema, ambao wameliongoza kwa vipindi
viwili vya mwaka 2000 hadi 2005 na baadae mwaka 2010 hadi sasa. Kama
hakutakuwa na mizengwe ndani ya chama chetu, Mbowe ataanguka katika
uchaguzi mkuu ujao,” alisema.
Wazee waliojitokeza kumfuata na kumshawishi Malya ni wa vijiji vya
Mungushi, Sanya Station, Rundugai, Mnadani, Machame Kusini, MailiSita na
Kalali.
Hata hivyo, Malya alipoulizwa na NIPASHE kuhusu hatua hiyo ya
wakazi wa Wilaya ya Hai, alikiri kufuatwa na baadhi ya wazee
wakimshawishi kutangaza nia ya kugombea ubunge katika jimbo hilo kwa
tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Uchaguzi Mkuu ujao. "Ni kweli
walikuja wazee wa Hai, huku mkoani Arusha na kuniomba niende nikagombee,
nikawaeleza kwamba natafakari lakini nikawaahidi kwamba wakati ukifika
nitatangaza nia hiyo," alisema Malya
إرسال تعليق