Mwanasheria
Mkuu wa Serikali (AG) mstaafu, Jaji Mark Bomani, ambaye pia ni mtaalam
nguli wa Katiba, ameonya kuwa iwapo upigaji wa kura ya maoni ya Katiba
inayopendekezwa utalazimishwa kufanyika Aprili 30, mwaka huu, wakati
dalili zote zinaonyesha kuwa haiwezekani, unaweza kuzua mtafaruku mkubwa
nchini.
Ili
kuepusha hali hiyo, ameshauri kura ya maoni iahirishwe hadi baadaye,
badala yake Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) iendelee na uboreshaji wa
daftari la kudumu la wapigakura kwa ajili ya kutumika katika uchaguzi
mkuu wa Oktoba, mwaka huu.
Pia,
amependekeza kuwa Katiba inayotumika sasa ya mwaka 1977 iboreshwe kwa
kuingiza ndani yake mambo mbalimbali, akiwamo mgombea binafsi.
Jaji
Bomani ambaye ni mtaalam nguli wa Katiba aliyewahi kuandika katiba za
nchi mbalimbali, zikiwamo za Namibia na Burundi, alisema hayo
alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.
Alisema
nia nzuri ya Rais Jakaya Kikwete, ya kuipatia Tanzania Katiba mpya,
iliharibika baada ya kuundwa kwa Bunge Maalum la Katiba (BMK).
Jaji Bomani alisema hilo lilidhihirika baada ya baadhi ya wajumbe wa BMK kujitoa katika Bunge hilo.
“Hili lilikuwa doa kubwa sana kwa mchakato wote. Ilikuwa ni mwanzo mbaya,” alisema Jaji Bomani.
Aliongeza: “Kazi yake (BMK) haikuwa nzuri, haikuridhisha, kwani iliwagawa watu.”
Alisema
licha ya baadhi ya wajumbe wa BMK kubaki kwenye Bunge hilo na kuendelea
na mchakato hadi kutoa Katiba inayopendekezwa, bado anaona kuna
matatizo mawili.
La kwanza,
alisema ni kuwapo baadhi ya makundi na watu wanaoamini kuwa Katiba
inayopendekezwa imetupilia mbali baadhi ya mambo yaliyopendekezwa na
iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba yaliyotokana na maoni ya
wananchi, hivyo wanaipinga na baadhi yao wanatishia kutoipitisha.
“Hili
ni jambo la kusikitisha, lakini siyo jambo la kupuuza. Katiba siyo kitu
kinachotegemea kura, bali inatakiwa iwe na muafaka. Kitu hicho Katiba
za Namibia na Burundi inacho,” alisema Jaji Bomani.
Alisema katiba ya nchi ndiyo sheria mama na msingi wa kuendesha nchi na kwamba uzuri wake, sharti uungwe mkono na wengi.
Alisema Katiba inayopingwa na kundi kubwa la watu, ni chanzo cha mfarakano kwenye nchi.
Alisema
endapo katiba ya namna hiyo inapigiwa kura nyingi za `hapana' au
inapingwa na upande mmojawapo wa Muungano iwe Zanzibar au Tanganyika,
basi hatima yake ni kuvunja Muungano na kuhoji: “Je, ni sawa tufike
huko?”
La pili,
alisema ana wasiwasi mkubwa juu ya uwezekano wa kura hiyo kupigwa
Aprili 30, mwaka huu, kwani hadi kufikia jana uandikishaji wa wapigakura
katika daftari la kudumu la wapigakura ulikuwa ukisuasua.
“Naambiwa
eti mpaka sasa waliokwishaandikishwa hawazidi hata milioni moja. Hapo
takriban zaidi ya milioni 20 wataandikishwa katika wiki nne zilizobaki?
Nafikiri itakuwa ni muujiza kufanya hivyo,” alisema Jaji Bomani.
Aliongeza: “Sasa
tufanyeje? Tuendelee na kura ya maoni ambayo ni idadi ndogo ya
wapigakura walioandikishwa ndiyo watakaoshiriki, tena kwa suala zito
kama la Katiba? Tukifanya hivyo tutakuwa tumefanya kosa kubwa sana
ambalo litatuletea mgogoro mkubwa na manung’uniko mengi sana nchini.
Hivi kweli tufike hapo?”
“Mapendekezo
yangu ni kwamba kura ya maoni juu ya Katiba mpya iahirishwe mpaka
baaadaye. Badala yake Tume ya Uchaguzi iendelee na uboreshaji wa daftari
la wapigakura tayari kwa uchaguzi mkuu Oktoba 2015. Ikiwezekana hata
tuachane na mfumo wa BVR (mfumo mpya wa kielektroniki wa Biometric
Voters Registartion), ambao umewapa shida hata wenzetu Kenya na
Nigeria.”
Hata
hivyo, alisema kwenye rasimu ya iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba
na Katiba inayopendekezwa, kuna mambo mazuri, hivyo akashauri yafanyiwe
mabadiliko katika iliyopo ili yatumike kwenye uchaguzi wa Oktoba, mwaka
huu.
Aliyataja
baadhi ya mambo hayo kuwa ni pamoja na uwakilishi sawa wa jinsia,
mgombea binafsi, mgombea urais kupata asilimia 50 au zaidi ili ashinde
na Tume Huru ya Uchaguzi.
“Katiba
iliyopo inaweza kufanyiwa mabadiliko haraka haraka, tuseme kwenye kikao
kijacho cha Bunge tayari kwa matumizi ya uchaguzi mkuu ujao. Litakuwa
ni jambo la kusikitisha kuwa hata yale mazuri yasiyo na ubishi
yasitumiwe kwenye uchaguzi huo,” alisema Jaji Bomani.
Aliongeza:
“Unahitajika muda zaidi wa mazungumzo. Kwani Watanzania tunataka nini
au Mtanzania wa kawaida anataka nini? Anataka maisha yake yaboreke,
hawataki Muungano wa serikali mbili, tatu wala moja, hivyo ni vitu vya
uongozi, havitakiwi uhasama.”
Alisema
kura ya maoni haiwezekani kufanyika Aprili 30, mwaka huu kwa kuwa
maandalizi hayajafanyika ya kutosha, kwani wapigakura kati ya milioni 20
hadi 23 wanaotarajiwa wanatakiwa wote wapewe nafasi ya kupiga kura.
“Ukiangalia
kwenye maandalizi, hatujafika hata nusu. Nina wasiwasi kama hiyo tarehe
30 itafika wote watakuwa wameandikishwa. Tulipe muda. Tusijiongeze kitu
kitakachoongeza mfarakano,” alisema Jaji Bomani.
إرسال تعليق