Mjumbe wa Baraza la Wadhamini wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon
Ndesamburo, amepanga kuwasilisha hoja binafsi bungeni, akiitaka Wizara
ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kutoa maelezo kuhusu Jeshi la Polisi
kushindwa kuwakamata watuhumiwa wanne wa mauaji ya kukusudia ya
aliyekuwa meneja wa baa moja maarufu mjini hapa, James John.
James aliuawa Juni 06, mwaka 2009 na watu wanne wanaodaiwa kuwa
ndugu wa familia moja, huko katika Kijiji cha Kindi-Kibosho, Wilaya ya
Moshi.
Jana, Ndesamburo alisema katika hoja yake atamtaka Waziri wa Mambo
ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, kulieleza Bunge sababu zinazolifanya
Jeshi la Polisi kushikwa na kigugumizi cha kuwakamata watuhumiwa hao na
kuwafikisha mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
“Katika maelezo ya hoja hiyo, nitataka pia serikali kueleza lilipo
jalada la uchunguzi wa mauaji hayo. Nimeamua kuchukua uamuzi huu, kwa
kutumia Ibara ya 63 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya
mwaka 1977, ambayo imelipa Bunge, Mamlaka ya kuishauri na kuisimamia
Serikali na vyombo vyake katika kutekeleza majukumu yake,” alisema
Ndesamburo.
Alisema yeye kama Mbunge wa Moshi Mjini, ambaye amekuwa akiheshimu
utawala wa sheria, ameamua kulichukua jambo hilo na atalipeleka bungeni
baadaye mwezi huu ili kulisukuma Jeshi la Polisi liwajibike kutekeleza
wajibu wake.
Jeshi la Polisi liliwakamata na kuwafungulia mashtaka ya mauaji,
watu wawili tofauti (Majina yao yamehifadhiwa), ambao hata hivyo,
waliachiwa huru na Mahakama baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini
(DPP), kudai hakukuwa na ushahidi wa kutosha wa kuwatia hatiani
watuhumiwa hao.
Wakati, Ndesamburo akijitwisha msalaba huo, baadhi ya ndugu wa
marehemu James wamemwomba Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Ernest
Mangu, kuingilia kati sakata hilo ili kutoa msukumo utakaopelekea
kukamatwa kwa watuhumiwa wanne wanaodaiwa kuhusika katika mauaji hayo
إرسال تعليق