Nyaraka za kale za mikataba ya kimataifa ya Zanzibar na Ujerumani,
inayohusu umiliki wa Zanzibar katika eneo la mwambao wa Pwani ya Afrika
ya Mashariki kuanzia Mombasa hadi Kilwa, zimeibwa katika Nyumba ya
Nyaraka Kilimani.
Nyaraka hizo zinadaiwa kuibwa na ofisa mmoja wa Ubalozi wa Oman kwa
utashi wake na si kwa amri ya Serikali ya Oman, kama ilivyodhaniwa na
baadhi ya watu.
Hayo yalielezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais,
Mohamed Aboud, wakati akitoa ufafanuzi kuhusu suala hilo, ambalo
limekuwa likiandikwa kwa mtazamo tofauti, kiasi cha kupoteza ukweli
wake.
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walipokea ripoti ya wizi wa nyaraka,
iliyowasilishwa na Mwakilishi wa Jimbo la Kikwajuni, Mahmoud Mohamed
Mussa (CCM), ambayo ilimtaja Ofisa Mwandamizi wa Ubalozi Mdogo wa
Oman, Zanzibar, Humud, kuhusika na tukio hilo kwa kurubuni wafanyakazi
wa ofisi ya nyaraka.
Taarifa hiyo ilisema wizi wa nyaraka, ulifanyika katika nyakati
tofauti kwa kuwahusisha wafanyakazi hao, ambao walikuwa wakishirikiana
na karibu na ofisa mwandamizi wa ubalozi mdogo wa Oman uliopo Zanzibar.
Kutokana na taarifa hiyo, Aboud alisema wizi wa nyaraka mbalimbali za
kale, uliofanywa katika nyumba ya nyaraka iliyopo Kilimani, ulifanywa
kwa utashi wa ofisa mmoja wa ubalozi huo na sio kwa maelekezo ya
Serikali ya Oman.
Alisema wizi huo kwa kiasi kikubwa umesababisha upungufu mkubwa wa
nyaraka muhimu katika nyumba ya nyaraka Kilimani, ambazo hutumiwa kwa
ajili ya kufanya utafiti wa mambo ya kale na wanafunzi wa masomo ya
elimu ya juu .
“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatoa ufafanuzi wa suala la upotevu wa nyaraka katika nyumba ya nyaraka Kilimani na kwamba Serikali ya Oman haihusiki na wizi huo ambao umefanywa na mtu mmoja kwa utashi wake,”alisema.
“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatoa ufafanuzi wa suala la upotevu wa nyaraka katika nyumba ya nyaraka Kilimani na kwamba Serikali ya Oman haihusiki na wizi huo ambao umefanywa na mtu mmoja kwa utashi wake,”alisema.
Alisema Serikali inafuatilia suala hilo kwa karibu zaidi ili
kuhakikisha nyaraka zilizoibwa, zinarudishwa na wahusika ikiwemo baadhi
ya watumishi wa Serikali, wameanza kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
Aboud alisema Zanzibar ni miongoni mwa nchi, ambazo zimebahatika kuwa
na nyaraka muhimu za mambo ya kale katika utawala wa Kisultani na
utawala wa Uingereza na Ujerumani katika mikataba yake.
Alifafanua kuwa Serikali ya Oman imetoa misaada mingi kwa Zanzibar,
ikiwemo ya kuimarisha majengo ya kale, makumbusho na nyaraka ili kuwepo
kwa uhifadhi wa nyaraka sahihi kwa ajili ya kukuza maendeleo ya sekta ya
utalii.
“Serikali ya Oman inatekeleza makubaliano ya kuimarisha mambo ya kale
na makumbusho kwa ajili ya kuweka utaratibu mzuri utakaosaidia
kuimarisha utalii,” alisema

إرسال تعليق