PICHA:- HIVI NDIVYO MSAADA WA HARAKA ULIVYOITAJIKA LAMADI BAADA YA MAFURIKO KUTOKEA - INATISHA SANA!!

 Nyumba ikiwa imezingirwa maji huko Lamadi ambapo zaidi ya wakazi  300 wa kijiji cha Lamadi Wilayani Busega mkoani Simiyu hawana sehemu za kuishi kutokana na nyumba zao kusombwa na maji kufuatia mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali kunyesha jana-Picha na Simiyu
 Nyumba zikiwa zimezingirwa maji
 Hali ni mbaya
 Nyumba iliyoezekwa kwa nyasi ikiwa imebomolewa na mvua
 Nyumba iliyoezekwa kwa nyasi ikiwa imebomolewa na mvua
 Nyumba ya kienyeji ikiwa imezingirwa maji huko Lamadi Simiyu
*****
Zaidi ya wakazi  300 wa kijiji cha Lamadi Wilayani Busega mkoani Simiyu hawana sehemu za kuishi kutokana na nyumba zao kusombwa na maji kufuatia mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali kunyesha jana majira ya usiku.

Mvua hiyo ilisababisha mafuriko makubwa ambayo yaliyosababisha nyumba zao kuingiliwa na maji na nyingine kuezuliwa na upepo mkali.

 Baadhi ya wakazi wa kijiji hicho wamehifadhiwa na ndugu na jamaa zao huku wengine wakikimbilia katika taasisi za serikali ikiwemo shule ya msingi Nyamajeshi iliyopo kijijini hapo kwa ajili ya usalama wa maisha yao.

Akizungumza katika eneo la tukio diwani wa kata ya Lamadi Emanuel Desera alisema  tukio hilo limetokea  baada ya mvua hiyo kunyesha kwa muda mrefu hali iliyosababisha maji yazidi kujaa katika maeneo ya wakazi ya watu na kusababisha nyumba nyingi kubomoka.

Desera alisema baada ya mvua hiyo kufanya uharibifu huo wananchi hao walilazimika kukimbilia katika maeneo yaliyo salama ambapo ni shule ya msingi Nyamajashi ili  kunusuru maisha yao kutokana na nyumba zao kujaa maji.

Alibainisha kuwa hali ya wananchi hao kwa hivi sasa siyo nzuri kwani wahanga  wengine wamekimbilia kwa ndugu zao kujihifadhi, huku akibainisha kuwa mafuriko bado yanaongezeka na kuiomba serikali kupeleka msaada wa chakula madawa na mahema kwa wahanga hao.

“Vitongoji vilivyokumbwa na mafuriko hayo ni Kisesa,Sokoni Mwalukonge,Lukungu,Iseni B na Mwabayanda ambapo nyumba 200  zimesombwa na maji na watu zaidi ya 300 wapo katika shule ya msingi Nyamajashi ili kuweza kujinusuru na mvua”,alisema Desera.

Mmoja wa wakazi wa jiji cha Lamadi  Joseph Chenga ameiomba serikali kupitia ofisi ya waziri mkuu kupeleka misaada ya mahema na chakula ili kuwawezesha wananchi hao kupata chakula kwani mpaka sasa chakula walichokuwa wakikitegemea kimesombwa na maji katika makazi yao.

Baadhi ya wananchi hao wakiongea na waandishi wa habari waliofika katika tukio hilo walisema kuwa maji hayo yamejaa kutokana na vijiji hivyo kuwa kwenye bonde hali ambayo mvua zikizidi maji hutuama na kukosa sehemu ya kuelekea hivyo yanarudi katika makazi ya watu.

”Mvua hiyo ilianza kunyesha majira ya saa sita usiku ambapo maji yalijaa katika nyumba na kusomba vitu mbalimbali pamoja na kuku hali iliyotulazimu kukimbilia katika katika shule ya msingi Nyamajashi kwa ajili ya kujihifadhi,pamoja na kupata msaada zaidi kutoka serikalini”,alisema mmoja wa waathirika wa mafuriko.

Viongozi mbalimbali wakiwemo kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo ikiongozwa na mkuu wa polisi wa wilaya walifika eneo la tukio na kujionea uharibifu huo ikiwa pamoja na kuangalia usalama wa wananchi hao waliokumbwa na mafuriko hayo.

Post a Comment

Previous Post Next Post