Dar es Salaam. Zaidi ya Sh 1.2 trilioni zimetolewa na wadau wa
maendeleo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maboresho ya Bandari ya
Dar es Salaam inayofanywa chini ya Mpango wa Matokeo Mkubwa (BRN)sasa.
Miradi hiyo ambayo utekelezaji wake utaanza kesho
itafanywa kwa awamu mbili ambapo inatarajiwa kukamilika ndani ya mwaka
huu na mwaka ujao.
Akizungumza lleo kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi,
Samuel Sitta, wakati wa uzinduzi utekelezaji wa awamu ya kwanza ya
miradi hiyo Katibu Mkuu wa wizara hiyo Dk Shaaban Mwinjaka amesema,
fedha hizo zitatumika kwenye miradi ya maboresho ya miundombinu ya
bandari.
Amesema, sekta ya uchukuzi hasa bandari inakuwa
kwa kasi hivyo miundombinu yake lazima iboreshwe ili iende sambamba na
mabadiliko hayo.
“Tunataka ifikapo 2020 bandari iwe na uwezo wa kuingiza mizigo kutoka tani milioni 13 hadi tani 22 milioni.”
Amesema, fedha zilizotolewa na wadau hao zitatumika kwa mgawanyo kulingana na miradi.
“Utekelezaji wa awamu ya kwanza ambayo ni kubomoa
ghala mbili za bandarini na kuboresha barabara ndani ya bandari
umefadhiliwa na TradeMark Africa (TMEA).”amesema
Ameongeza, “Awamu ya pili itafadhiliwa na Benki ya Dunia (WB) pamoja na Idara ya Maendeleo ya Kimataifa (DFID).”
Akizungumzia mchango wao Mkurugenzi Mtendaji wa
TMEA, David Stanton amesema, wametoa Sh 108 bilioni kwa ajili ya kubomoa
ghala hizo.
“Fedha hizo zitasaidia kwenye kazi iliyoanza leo
ambayo itaendelea hadi mwezi ujao kwa ajili kuboresha eneo hili ambalo
litaanza kutumika kama sehemu ya kuweka kontena na siyo ghala
tena.”amesema Stanton.
Naye, mwakilishi kutoka WB Monthe Biyoud amesema,
benki yao pamoja na DFID watatoa Sh 873 bilioni kwa ajili ya utekelezaji
mradi wa awamu ya pili.
Amesema hadi kufukia Desemba mwaka huu wanatarajia fedha hizo zitakuwa zimeshatolewa.
إرسال تعليق