Naibu Waziri wa Nishati na Madini na mbunge wa jimbo la Misungwi mkoa wa Mwanza, Mh. Charles Kitwanga,akizungumza na wachimbaji wadogo wa dhahabu wa vijiji vya Mang’onyi na Sambaru wilaya ya Ikungi. Kitwanga amewataka wachimbaji hao kujiunga kwenye vikundi ili waweze kupata misaada mbalimbali ikiwemo kukopesheka na taasisi za kifedha.
DSC05010
Mkuu wa wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Gishuli Charles, akizungumza kwenye mkutano wa hadhara ulioitishwa kwa ajili ya Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Kitwanga kuzungumza na wachimbaji wa wadogo wa dhahabu katika vijiji vya Sambaru na Mang’onyi. Wa pili (aliyeketi) ni Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mh. Charles Kitwanga na anayefuatia ni mkuu wa wilaya ya Manyoni, Fatuma Toufiq.
DSC05014
Mjumbe wa halmashauri kuu CCM (NEC) wilaya ya Ikungi mkoa wa Singida, Jonathan Njau, akizungumza kwenye mkutano wa hadhara ilioitishwa kwa ajili ya Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mh. Kitwanga kuongea na wachimbaji wadogo wa dhahabu wa vijiji vya Sambaru na Mang’onyi.
DSC04988
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mh. Charles Kitwanga (katikati), akikagua madini aina ya Gypsum yanayochimbwa Itigi wilaya ya Manyoni. Madini hayo yanayochimbwa na wanawake, yanatumika kutengenezea saruji, chaki, gypsum board na P.O.P. Kulia ni aliyekuwa mbunge wa jimbo la Manyoni magharibi katika miaka ya nyuma, Ivatta na kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Manyoni, Fatma Toufiq.
DSC05004
Baadhi ya wachimbaji wadogo wa dhahabu wa vijiji vya Sambaru na Mang’onyi wilaya ya Ikungi,wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mh. Charles Kitwanga. Kitwanga amewaonya wachimbaji hao wasivamie mgodi wa dhahabu ya kampuni ya Shanta.
DSC04953
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mh. Charles Kitwanga (wa tatu kushoto) akizungumza ofisini kwa Mkuu wa mkoa wa Singida Dk.Parseko Kone (anayeangalia kamera) wakati akiwa kwenye ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani hapa.
DSC04954
Baadhi ya maafisa wa serikali mkoani Singida, wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati na Madini Mh. Charles Kitwanga (hayupo pichani) wakati akizungumza na Mkuu wa mkoa wa Singida, Dk.Parseko Kone ofisini kwake (anayeangalia kamera).(Picha zote na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu, Singida  
NAIBU Waziri wa Nishati na Madini, Mh. Charles Muhangwa Kitwanga (Mb), amewaonya wachimbaji wadogo wa dhahabu wasithubutu kuvamia mgodi wa dhahabu wa kampuni ya uchimbaji ya Shanta uliopo kijiji cha Sambaru wilayani Ikungi, na kwamba atakayekiuka agizo hilo atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Amesema kampuni ya uchimbaji madini ya Shanta, imemilikishwa kisheria mgodi huo na  inatarajia kuanza rasmi uchimbaji septemba mwaka huu.
Kitwanga mbunge wa jimbo la Misungwi mkoa wa Mwanza, ametoa onyo hilo wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na wachimbaji wadogo wa vijiji vya Sambaru na Mang’onyi waliyani Ikungi.
Alisema serikali imekuwa ikitoa leseni za uchimbaji madini kwa kuzingatia sheria na leseni hizo zipo katika makundi matatu ambayo ni leseni ya wachimabji wadogo,kati na wale wakubwa.
“Wachimbaji wadogo wanapewa leseni inayozingatia uwezo wao mdogo na wachimbaji wa daraja la kati,nao leseni zao zinazingatia uwezo wao.Wachimbaji wakubwa ni wale wenye mitaji mikubwa na wanatumia mitambo mikumbwa katika shughuli zao za uchimbaji”,alisema.
Akifafanua,naibu waziri huyo alisema sio busara kumpa leseni mchimbaji mdogo mahali eneo husika linahitaji mitambo mikubwa na mitaji mikubwa akidai kwamba hataweza kufanya lo lote.
“Nimesikia kilio chenu kwamba kwa sasa mnashindwa kusomesha watoto wenu na msimu huu mnakabiliwa na njaa kali,kwa hiyo Shanta iwape kitalu namba moja, ili mchimbe dhahabu yake mmuweze kupata fedha za kumaliza matatizo hayo.
Nawahakikishia ombi lenu hilo ni ngumu na halikubaliki kwa sababu Shanta ana leseni halali ya kumiliki eneo hilo,hatua mbadala ni kuwapa maeneo ambayo hayana wamiliki”,alifafanua zaidi.
Hata hivyo,alisema wanaendelea kushauriana na Shanta ili waweze kutoa eneo lao lililopo katika kijiji cha Mhintiri wilaya ya Ikungi lenye maeneo 7,000 ya kuchimba dhahabu, ili wachimbaji wadogo waweze kumilikishwa na kupatiwa leseni halali.
“Ninyi wachimbaji wadogo wa kijiji cha Sambaru na Mang’onyi,mna tatizo na mbaya zaidi mnakubali kupotoshwa na kuchonganishwa na serikalai yenu.Mnatakiwa mkiambiwa kitu na ninyi mchanganye na akili zenu kupambanua mbele ya safari nini kinaweza kutokea”,alisema na kuongeza kwa kusema;
“Angalieni Shanta imekipa kikundi cha uchimbaji cha Aminika msaada wa zaidi ya shilingi 42 milioni zisaidie kikundi hicho kijiendeleza kiuchimbaji,lakini kilichofanyika mnakijua.Mkibebwa hambebeki,badilikeni kwa kuanzisha vikundi ili iwe rahisi kukopesheka na kupewa misaada mingine ikiwemo mafunzo ya namna  kuboresha katika utendaji wenu”.
Aidha,alisema Shanta itakapoanzisha uzalishaji septemba mwaka huu,itatoa ajira nyingi kwa vijana na wakazi wa wilaya ya Ikungi na mkoa kwa ujumla.
Akisisitiza zaidi, Kitwanga alisema sio ajira tu,vile vile itasaidia kuboresha sekta ya afya,elimu na maji.
Wakati huo huo, naibu waziri huyo amemwomba mjumbe wa halmashauri kuu CCM (NEC) wilaya ya Ikungi, Jonathan Njau, kusaidia utaalamu wa kisheria bure kwa wachimbaji madini watakaounda vikundi vya uchimbaji madini.