Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote imesaini mkataba na
Kampuni za Mawasiliano kwa ajili ya kuziunganisha shule 250 za Serikali
na intaneti pamoja na kuanzisha vituo 25 vya kuwafundishia walimu.
Utekelezaji wa mradi huo wa mafunzo ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (Tehama) kwa kuunganisha shule, unategemewa kukamilika ndani
ya mwaka huu.
Hayo yalibainishwa Dar es Salaam jana na Waziri wa Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa alipokuwa akizungumza na
wadau na Kampuni za mawasiliano nchini.
Waziri Mbarawa alisema katika kipindi cha mwaka jana, Kampuni za simu
za Voda na Tigo, hazikukamilisha ujenzi wa mawasiliano waliokubaliana
katika zabuni walizopewa hivyo aliagiza kampuni hizo, kukamilisha ujenzi
huo katika kipindi hiki licha ya kwamba wameshafunga mkataba wao mwaka
uliopita.
Pia alisema kuwa kuna maeneo nchini, ambayo mpaka sasa yana matatizo
ya mawasiliano na kwamba wameingia mkataba na kampuni zote za
mawasiliano Tigo, Voda, Airtel na TTCL ili kuhakikisha tatizo hilo
linatoweka.
‘’Pamoja na mambo mengine, leo pia tumesaini mkataba wa kupeleka
mawasiliano vijijini katika Kata 102 mradi wa awamu ya pili A (2A)
ambapo ruzuku ni Sh bilioni 14.2 na kata 10 za mradi wa mawasiliano
mipakani na maeneo maalumu ruzuku ni Sh bilioni 2.7,’’ alisema Profesa
Mbarawa.
Akizungumzia fursa ya wazawa katika ununuaji wa hisa zinazotolewa na
kampuni za mawasiliano, Waziri huyo alisema kuwa wameshaandaa kanuni
ambazo zitawasaidia wazawa kuweza kuingia katika ununuaji wa hisa, ili
kuhakikisha Kampuni za mawasiliano nchini hazirudi nyuma katika kutoa
huduma.
Alisema kuwa kanuni hizo zinatarajiwa kutangazwa ndani ya mwaka huu
na kwamba wataangalia jinsi ya kuwawezesha wazawa kufanikiwa pamoja na
kuongeza mitaji kwa kampuni za mawasiliano kupitia hisa hizo.
“Serikali imeshirikiana na Benki, Soko la hisa Dar es Salaam, Kampuni
za simu kuandaa kanuni hizo ambazo zitasaidia kuhakikisha wanakua
kimaendeleo na sio kushuka kiuchumi,’’ alifafanua.
Aliongeza kuwa ipo haja ya Watanzania wenyewe kuhakikisha wanakuwa
mstari wa mbele katika kununua hisa ili wasiwe na kisingizio cha kwamba
wageni ndio wananufaika na hisa zinazotangazwa.
‘’Kama tusipokuwa makini ni lazima tutaona kuwa wageni wananufaika na
hisa zinazotangazwa. Hivyo tunaandaa kanuni ili kuhakikisha na wazawa
wanakuwa mstari wa mbele kununua hisa hizo,’’ alisema.
Post a Comment