Watuhumiwa
wanne wamekamatwa jijini Dar es Salaam katika makutano ya barabara ya
Bibi Titi na Ohio karibu na Hotel ya Serena baada ya kumpora raia wa
kigeni wakiwa na gari dogo rangi ya kijivu yenye nambari za usajili T787
DBU Toyota Cienta.
Hivi
karibuni kumeibuka wimbi la wahalifu kuwapora pesa na vitu vya thamani
kama mikufu, bangili, hereni pia pete na vitu mbalimbali vya thamani
raia wa kigeni na akina mama ambao hupenda kutembea na pochi. Wahalifu
hawa hutumia gari dogo ambalo mara kwa mara hubadilishwa namba zake za
usajili na wakati mwingine gari hili wanalitumia kama Tax bubu.
Leo
tarehe 21/04/2015 majira ya saa 09:00 asubuhi katika eneo la Posta Mpya
watuhumiwa hawa walimdangavya bwana CEES S/O JAN CONIJN, Miaka 27, raia
wa Uholanzi aliyetaka kufika Klabu ya Leaders kwamba wangempeleka eneo
hilo kwa kutumia gari tajwa hapo juu. Baada ya kuondoka na dereva kila
baada ya mita 200 dereva huyo alikuwa anasimamisha gari na kuongeza mtu
mwingine kama abiria hadi walipotimia wote wane.
Walimpeleka
hadi maeneo ya Kinondoni kwa Manyanya na walipofika eneo hilo
walimweleza wazi kuwa wao ni wahalifu na walimtaka awapatie pesa
vinginevyo wangemuua. Aliwapatia pesa zote alizokuwa nazo Tshs 75,000/=
lakini hawakuridhika ndipo walipomtaka awapatie kadi ya benki (ATM CARD)
na nambari za siri (Pass Word).
Baada
ya tukio hilo wakamtupa karibu na Hospitali ya Mwananyamala na wao
wakageuza gari kurudi katikati ya mji. Wakati tukio hilo linatokea raia
wema walishuhudia na kutoa taarifa kwa Polisi. Polisi walifuatilia
haraka na kuweka mtego uliowanasa watuhumiwa wote katika eneo la
makutano ya barabara ya Bibi Titi na Ohio karibu na Hotel ya Serena.

Majina ya watuhumiwa waliokamatwa ni:
1. SALUM S/O SAID MTUMWA @ MARO, Miaka 25, Mkazi wa Chang’ombe Bora.
2. ALEX S/O INNOCENT MANGUKA @ MAKA, Miaka 30, Mkazi wa Kimara Temboni.
3. MOHAMED S/O ALLY ABDALLA @ MEDY, Miaka 27, Mkazi wa Mwananyamala.
4. STEPHANO S/O ALBERT KIKINDI @ KING, Miaka 32, Mkazi wa Mwananyamala.
Walipopekuliwa
watuhumiwa hawa walikutwa na simu mbalimbali za mkononi zipatazo 11
ambazo zinachunguzwa kuhusiana na mbinu ya uhalifu wanaoutumia. Pia
ilikamatwa ATM CARD iliyochukuliwa kwa mlalamikaji kabla watuhumiwa hao
hawajaitumia. Aidha gari namba T787 DBU Toyota Cienta linashikiliwa kwa
uchunguzi zaidi.
Miongoni
mwa watuhumiwa waliokamatwa, wawili ambao ni MOHAMED S/O ALLY ABDALLA @
MEDY, na STEPHANO S/O ALBERT KIKINDI @ KING, tayari wanazo kesi
nyingine mahakamani na wako nje kwa dhamana.
Sambamba
na tukio hili oparesheni ya kuwakamata wahalifu wengine wenye mtindo
huu wa kuwapora wageni au wakina mama wenye mikoba inaendelea na
tunawaomba wananchi waonyeshe ushirikiano wa kutosha ili kutokomeza
vitendo hivyo viovu. Aidha hakuna silaha yoyote iliyotumika au kukamatwa
kama ilivyoripotiwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii.
S. H. KOVA,
KAMISHNA WA POLISI KANDA MAALUM,
DAR ES SALAAM.
Post a Comment