Katibu wa Halmashauri Kuu (Nec), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye.
Tofauti na miaka yote, chama hicho kikongwe kimekuwa kikitangaza
ratiba mapema kuwawezesha wanachama wake kufahamu utaratibu wa kuchukua
fomu ya kuomba kuteuliwa kuwania uongozi ndani ya Chama kupambana na
vyama vingine.
Hali hiyo ilibainika jana baada ya Katibu wa Halmashauri Kuu (Nec),
Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, kuzungumza katika mahojiano na NIPASHE
iliyotaka kujua lini kazi ya kuchukua fomu kwa wanachama wake wanaotaka
kuwania uongozi mwaka huu.
Nnauye alisema kipenga kwa ajili ya kuchukua fomu za udiwani,
ubunge na urais kitaanza pale vikao vitakapokaa na kuamua bila kutaja
tarehe rasmi lini vitakaa.
“Pale vikao vitakapokaa na kuamua hivyo ndipo kipenga kitapulizwa, kwa sasa bado vikao havijapangwa," alisema.
Ukimya huu wa CCM unazidi kuleta wasiwasi hasa kwa wanachama wake
sita ambao Februari, mwaka jana walipewa adhabu ya mwaka mmoja
wasijihusishe na kampeni mapema lakini hadi sasa adhabu yao
haijatenguliwa.
Makada hao walioitwa na Kamati Ndogo ya Nidhamu iliyokuwa
ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Philip Mangula, na
kuwahoji kwa tuhuma za kuanza kampeni za uchaguzi mkuu ujao kabla ya
wakati.
Makada hao ni Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, Waziri Mkuu wa
zamani, Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen
Wasira, Mbunge wa Sengerema (CCM), Wiliam Ngeleja na Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba.
Wabunge wa CCM wakati wa mkutano wa 19 wa Bunge uliomalizika wiki
iliyopita, walikutana mjini Dodoma na kupendekeza Chama kifanye mchujo
wa wagombea na kubakisha majina matatu ambao watapigiwa kura ya maoni na
wanachama.
Aidha, wabunge ambao wametekeleza vizuri ilani ya uchaguzi,
walipendekeza chama kiwapitishe moja kwa moja na chama kuwania nafasi ya
ubunge na udiwani na kusiwepo na wagombea wengine kutoka CCM kupambana
na aliyopo sasa.
Utaratibu huo utatumika kwa wagombea wa nafasi ya udiwani,ubunge na
urais na imeelezwa kuwa utasaidia kupunguza tatizo la rushwa
inayotolewa kwa wajumbe wanaoshiriki mkutano wa kura ya maoni.
Mapendekezo hayo yalitolewa Machi 23, mwaka huu wakati wa mkutano
wa wabunge wa CCM uliofanyika ukumbi wa Msekwa mjini Dodoma kwenye
viwanja vya Bunge chini ya Uenyekiti wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na
Katibu wa Wabunge wa CCM, Jenister Mhagama.
Vyanzo vya habari kutoka ndani ya mkutano vilieleza kuwa wabunge
hao walisema utaratibu huo ukitumika siku ya kupiga kura, wajumbe
watakaokuwa wanapiga kura watapiga kwa siku moja kwa wagombea hao watatu
watakaokuwa wamependekezwa na Chama.
Kuhusu utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi, walisema wabunge ambao
majimbo yao yamefanya vizuri kutekeleza Ilani na uchaguzi wa serikali za
mitaa, wasiwekewe wagombea wengine wa ndani ya Chama kupambana nao
badala yake Chama kiwateue wawe wagombea katika majimbo yao.
Katika mkutano huo ilipendekezwa kuwa ili kujiridhisha kama mbunge
wa jimbo husika ametekeleza vizuri Ilani ya Uchaguzi, iundwe kamati
ndogo itakayojumuisha wajumbe wa kada mbalimbali wakiwamo maofisa
usalama ambao watapita kila jimbo kupata uhakika kama ilani imetekelezwa
na mbunge husika.
Kamati hiyo itaundwa kwa siri, itafika katika jimbo husika bila
kumfahamisha mbunge wa jimbo hilo na kufanya kazi yake ya uchunguzi.
Baada ya kumaliza kazi yake, kamati hiyo itatoa ripoti ya mambo
yaliyobainika katika jimbo hilo kwa Chama ambacho kupitia vikao vyake,
kitatoa taarifa kuwa mbunge huyo anapaswa kuwa mgombea pekee
atakayepeperusha bendera ya Chama kuchuana na mgombea kutoka chama cha
upinzani.
إرسال تعليق