Vigogo Chadema Handeni wasimamishwa uongozi.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
Baraza la Uongozi la Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Tanga, limewasimamisha uongozi Mwenyekiti, Katibu na wajumbe wa chama hicho Wilaya ya Handeni kwa madai ya kushindwa kuwajibika ndani ya chama pamoja.
 
Kadhalika, baraza hilo limechukua hatua kama hiyo kwa katibu wa chama hicho wilayani Muheza.
 
Akielezea hatua hiyo, Katibu wa Chadema mkoani Tanga, Ismail Masoud, alisema uongozi wa chama hicho umewasimamisha kazi viongozi hao hadi uchunguzi dhidi yao utakapomalizika.
 
Aliwataja viongozi hao kuwa ni Jadi Bamba, ambaye ni Mwenyekiti, Ibrahim Ramia (Katibu) pamoja na wajumbe sita wa Baraza la Uongozi.
 
Alisema viongozi hao wanakabiliwa na tuhuma za kushindwa kukisaidia Chama kunyakua nafasi za uenyekitiwa serikali za mitaa uliofanyika hivi karibuni na kuunda makundi ndani ya chama hicho.
 
“Baraza la Uongozi Chadema Mkoa, limepitisha uamuzi mmoja wa kuwasimamisha kazi Mwenyekiti, Katibu na wajumbe wote wa wilaya kwa tuhuma za kukihujumu Chama,” alisisitiza.
 
Alifafanua kuwa viongozi hao wamesimamishwa hadi uchuguzi dhidi ya tuhuma zao utakapokamilika.
 
Masoud alisema kutowajibika kwa makatibu kumesababisha kutoa mwanya kwa vyama pinzani kujiimarisha na kuchukua maeneo ambayo tayari yalikuwa na ushawishi mkubwa wa Chadema na kuwa na uhakika katika uchaguzi mkuu ujao kufanya vizuri nafasi za udiwani.

Post a Comment

Previous Post Next Post