Mambo 10 ya kujiokoa na shambulio la ugaidi

Dar es Salaam. Wakati mashambulizi ya kigaidi yakiendelea kutikisa maeneo mbalimbali duniani ikiwamo nchi jirani ya Kenya huku kukiwa na angalizo kuwa huenda na Tanzania ikashambuliwa, jarida moja la kimataifa limetaja mambo 10 ya kufanya baada ya shambulio.
Mambo hayo ambayo ni hatua za kumsaidia mtu aliyenusurika katika shambulio husika ili kunusuru maisha yake, yametajwa wakati zikiwapo taarifa za tisho la shambulizi katika miji ya Dar es Salaam na Mwanza.
Jarida hilo lilifanya mahojiano na wataalamu wa sayansi ambao walitoa mapendekezo ambayo mtu anaweza kufuata  wakati au baada ya mlipuko na kuwa asilimia 50 ya watu wanaokutwa katika mashambulizi ya kigaidi  hujeruhiwa na wengine kupoteza maisha kwa sababu hawafahamu jinsi ya kujihami.
Tanzania iliwahi kukumbwa na shambulio la ugaidi mwaka 1998 wakati Ubalozi za Marekani, jijini Dar es Salaam ulipolipuliwa na kusababisha vifo vya watu kumi na moja. Shambulio hilo lilitokea sambamba na lile la ubalozi wa nchi hiyo, Nairobi, Kenya lililosababisha vifo ya watu 213.
Uvumi zaidi umeendelea kuenea baada ya shambulio la kigaidi lililotokea wiki iliyopita katika Chuo Kikuu cha Garissa, Kenya na kuua  wanafunzi 148.
Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe alisema pamoja na kusikia taarifa hizo, mpaka sasa Serikali haijaweza kuthibitisha ripoti hizo zinazoenea, lakini inachukua tahadhari juu ya suala hilo.
Polisi, Serikali wajiandaa
Akizungumzia tahadhari mbalimbali za mashambulizi ya kigaidi au Watanzania kushiriki katika ugaidi, Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Diwani Athuman alisema hali hiyo ina taswira kuwa Taifa si salama kwa asilimia 100.
“Kuna usemi usemao mwenzako akinyolewa wewe tia maji, Tanzania si kisiwa, kuna changamoto kubwa kwa sababu tumepakana na wenzetu Kenya ambao wameathiriwa na ugaidi, ndiyo maana hatuwezi kusema tupo salama kwa asilimia 100,” alisema.
Alisema kutokana na hali ilivyo sasa, Watanzania hawana budi kutilia mkazo umoja kama njia ya kutokomeza uhalifu na kuacha kushabikia masuala ya ugaidi.
Kuhusu vijana kujiunga na makundi ya ugaidi, Diwani alisema wazazi hawana budi kuwafuatilia watoto huko shuleni ili wajue kinachoendelea.
“Tanzania ni lazima irudi kule ambako ilikuwa. Kila mmoja ni mlinzi wa mwingine, sasa hivi watoto wanaachwa hadi wanapumbazika na kujiunga na makundi ya ugaidi. Hii si kazi ya vyombo vya dola peke yake ni ya kila mmoja,” alisema

Post a Comment

Previous Post Next Post