Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) likiwa
ni msimamizi na mratibu wa sekta ya Sanaa nchini linapenda kutoa pongezi za
dhati kwa Wasanii wa muziki wa kizazi kipya Nassib Abdul maarufu kama Diamond,
Omary Faraji Nyembo maarufu kwa jina la Ommy Dimpoz na Vanessa Mdee maarufu kwa
jina la Vee Money kwa kushinda tuzo mbalimbali kwenye Tuzo za African Music Magazine
Awards (AFRIMMA) zilizofanyika jijini Dallas nchini Marekani.
Katika tuzo hizo Msanii Diamond
ameshinda tuzo tatu ambazo ni Video Bora ya Kucheza (Best Dance Video), Msanii
Bora wa Mwaka (Best Artist of the Year) na Msanii Bora wa Kiume wa Afrika
Mashariki (Best Male East African Artist). Aidha Ommy Dimpoz na Vanessa Mdee
wameshinda tuzo za Best New Artist in Africa (Msanii Bora Mpya Africa) na
Msanii Bora wa kike wa Afrika Mashariki (Best Female East African Artist)
sawia.
Kuteuliwa kwa wasanii wetu na
baadaye kushinda katika tuzo mbalimbali za Afrika na duniani ni ishara kwamba wasanii
wetu wanakubalika ndani na nje ya Tanzania na kwamba hawana budi kuhakikisha
wanatumia fursa hizi katika kupanua wigo wa fursa za masoko kitaifa na
kimataifa.
Baraza linatoa wito kwa wasanii na
wadau wote wa muziki kuzidisha ubunifu, nidhamu, bidii, mshikamano na weledi
katika kazi wanazozifanya ili wasanii wengi wa Tanzania waweze kuchomoza katika
tuzo na majukwaa mbalimbali ya kimataifa kwa lengo la kulitangaza Taifa na
kukuza soko la kazi zao.
Ni matumaini ya Baraza kwamba
wasanii wataendelea kutambua umuhimu wa kufanya kazi na mapromota wenye upeo na
mapenzi mema, kufuata Sheria, Kanuni na taratibu za kutambuliwa na Serikali na
zaidi kuhakikisha wanapokwenda nje ya nchi wanafuata taratibu zote sambamba na
kukabidhiwa bendera ya Taifa kama ishara ya uwakilishi wa Taifa letu.
SANAA NI KAZI
TUIKUZE, TUILINDE NA KUITHAMINI
Godfrey Mngereza
KAIMU
KATIBU MTENDAJI


Post a Comment