WA 3 WALIOFUNGIWA NDANI MIAKA 10 NA MAMA YAO MMOJA AFARIKI DUNIA

Katika Blog Yetu wiki iliyopita, kuliandikwa habari ya kusikitisha yenye kichwa kisemacho; "INASIKITISHA SANA!! MAMA AWAFUNGIA NDANI WANAYE 3 KWA MIAKA 10, Awachanganya Chumba Kimoja wa Kike na Kiume, Wapeana Mimba"
Ni habari ambayo ilizua gumzo kubwa nchini kutokana na mazingira yake kuwa ya kushtua.

Marehemu Ally Juma enzi za uhai wake.
Baada ya habari hiyo kutoka ambayo ilikuwa na lengo la kuisaidia familia hiyo, sasa habari mpya ni kwamba, mmoja wa watoto hao, Ally Juma amefariki dunia ghafla.
Marehemu Ally aliaga dunia bila kuugua usiku wa kuamkia Aprili 4, mwaka huu na kuzikwa Jumamosi iliyopita majira ya alasiri mazishi ambayo yalihudhuriwa na mamia ya wakazi wa Kijiji cha Kanga, Wilaya ya Mafia mkoani Pwani.
ALLY NI NANI?
Marehemu Ally ni miongoni mwa watoto watatu, wakiwemo Muhadia (wa kike) na Mzee ambaye alidaiwa kumpa ujauzito Muhadia ambaye ni dada yake kwa kuzaliwa.Uwazi lilifanikiwa kupata taarifa za kifo cha  Ally na kushiriki msiba huo ambapo  umati mkubwa wa wanakijiji walijitokeza, lakini cha kushangaza wengi walisema hawakuwa na taarifa za kufungiwa kwa watoto hao ndani kwa muda wa miaka 10.
Mwili wa Ally Juma ukipelekwa eneo la kaburi kwa ajili ya kuzikwa.
MAMA ASIMULIA
Mama wa watoto hao, Mwasiti Ally alipohojiwa juu ya kifo cha Ally alisema: “Huwa nina tabia ya kwenda kuwaangalia kila siku  usiku kabla ya kulala ili kujua wanaendeleaje  maana silali nao nyumba moja.
“Nilipofika nilimkuta Ally ametulia kama mtu aliyekata roho. Kwanza nilijua amelala, lakini nilipomwita na kumwona haitiki nikaanza kuingiwa na wasiwasi.
“Nilitoka kwenda kumtafuta jirani mmoja  na kumwambia kuhusiana na hali niliyomkuta nayo Ally. Tulikwenda wote. Ilikuwa kama saa 8 usiku. Kufika tukakuta amekata roho kweli. Ikabidi tuanze kutoa taarifa kwa majirani wengine.”
AMEKUFA KWA MAZINGIRA MAGUMU
Baadhi ya wanakijiiji walisema kuwa, kwa vile mama mtu anasema marehemu hakuonesha dalili zozote za kuumwa, wanaamini  kifo chake kilisababishwa na mazingira magumu, hasa ya kufungiwa ndani ya chumba kwa miaka mingi hivyo kukosa hewa safi, mionzi ya jua na kugusana na wadudu watambaao kila siku.
Muhadia ambaye ni dada'ke Ally.
WANACHOJUA WANAKIJIJI
Ally Makame mmoja wa wanakijiji hicho cha Kanga alisema kuwa watoto hao walianza kuteseka kwa miaka mingi lakini watu walipokuwa hawawaoni waliamini mama yao aliwasafirisha kwenda kuishi sehemu nyingine maana kikubwa kilichotawala dhidi ya matatizo yao ni imani za kishirikina.
“Kusema kweli wanakijiji wengi hatujui kama hawa watoto walikuwa wamefungiwa ndani kwa miaka yote hiyo mpaka tuliposoma kwenye Gazeti la Uwazi na hiki kifo kilipotokea.“Sisi tulipoacha kuwaona tuliamini mama yao aliwapeleka sehemu nyingine kuishi maana matatizo yao ushirikina ndiyo ulikuwa ukitajwa sana. Si unajua watoto watatu wa familia moja kuwa na matatizo ya akili haiingii akilini?
“Halafu watu wenyewe licha ya kuwa wagonjwa wa akili lakini walikuwa hawana ugomvi na mtu, ila sema ile tabia yao ya kutembeatembea ndiyo ilikuwa hatari kwa uhai wao,” alisema Makame.
HALI YA DADA NI TETE
Hali ya Muhadia ni mbaya huku watu wakihofia hatima yake, Mzee yeye kidogo ana nguvu na afya kiasi kwamba, muda mwingi hukimbia akiona watu kwa kuhofia kukamatwa.
Mzee Juma, anayedaiwa kumpa mimba dada yake wa kuzaliwa, Muhadia aliyejifungua mtoto akafariki.
UWAZI LAENDELEA KUKATA MBUGA.
Gazeti la Uwazi lilifanya jitihada za kumtafuta Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Dk. Nasoro Hamid ili aweza kutoa ufafanuzi juu ya familia hiyo ambapo alisema kuwa habari hiyo ameisoma kwenye mtandao na kutoa pongezi kubwa kwa Gazeti la Uwazi kwa kuiibua.
“Ndugu mwandishi ninachotaka kusema  ninatoa shukurani nyingi sana  kwa Kampuni ya Global Publishers kutuma mwandishi na kuweza kutoa habari kama  hiyo. “Kwanza  ni habari ambayo imekaa kipekee sana na mwandishi huyo bila kukata tamaa alifika katika kijiji hicho na kufanikiwa kupata  mahojiano na familia,” alisema mkuu huyo wa wilaya.
Ndugu jamaa na marafiki wakiwa na majonzi wakati wa msiba wa Ally.
Baada ya mahojiana na mwandishi wetu, DC huyo alisema amemwagiza Mkuu wa Idara ya Ustawi wa Jamii Wilaya ya Mafia kufika katika kijiji hicho ili aweze kupata maelezo ya kutosha kisha kutafuta namna ya kuisaidia familia hiyo.
Uwazi pia lilifika ngazi ya juu ambapo mwandishi wetu aliongea na Msemaji Mkuu wa Wizara ya Afya,  Nsachris Mwamwaja ambapo awali alilipongeza  Gazeti la Uwazi.“Gazeti nimeliona na habari yenyewe nimeisoma, ninampa ‘Big Up’ mwandishi kwa kufumua tukio kama hilo. Mafia ina serikali kamili hivyohivyo nina imani tatizo la familia ile litashughulikiwa kikamilifu na haraka iwezekanavyo,” alisema Mwamwaja.

Post a Comment

أحدث أقدم