WASIKILIZE UHARIBU MAISHA YAKO


KUNA msemo mmoja mashuhuri sana unasema mswahili atakunyima kila kitu, lakini si maneno, ambao hapa tunaweza kuutafsiri kama umbeya. Yes, waswahili kwa umbeya hawajambo, wanazungumza mambo hadi mwenyewe unashangaa, yaani wanakufahamu kuliko unavyojifahamu mwenyewe, hata kama mmefahamiana muda mfupi tu uliopita.
Siyo jambo baya kwa sababu ndiyo utamaduni tuliorithi kutoka kwa vizazi vilivyotangulia na kadiri dunia inavyobadilika, ile hali ya watu kujali zaidi maisha yao binafsi kuliko ya mtu, ndivyo utamaduni huu nao unavyozidi kufifia.
Zamani ilikuwa kawaida kukuta kijiwe cha kahawa kinaanza asubuhi hadi usiku, siku hizi ni vijiwe vya kuhesabu na hata wanaokaa kutwa nzima kijiweni wanazidi kupungua, ingawa idadi kubwa ni watu wenye umri mkubwa. Vijana wanapungua vijiweni kwa sababu wameshagundua hakuna mtu wa kuwasaidia maisha yao pasipo wenyewe kwenda spidi.
Lakini hali kidogo bado ngumu kwa akina dada. Wengi bado ni watu wa kupenda sana kuzungumzia maisha ya watu wengine, badala ya kuwa na muda mwingi wa kujadili maisha yao. Kwao, kila jambo linalofanywa na wanawake wenzao ni baya, hata kama ni zuri.
Nina ushauri mmoja kwa akina dada kwa sababu wao ndiyo waathirika wakubwa wa umbeya. Hii ni kwa sababu akinababa kidogo wana nafuu. Wanasikiliza na kushiriki umbeya, lakini hawajali, yaani kwao mambo yanaishia hapohapo kijiweni, wachache wanaoweka kichwani, ni wale ambao fainali imeshawakuta!
Shiriki umbeya, kwa sababu wakati mwingine hauwezi kuukwepa, lakini kuwa na akili ya ziada. Siyo kila utakaloambiwa ni baya, hapana.
Yapo mengine ni mazuri, yaweke na yafanyie kazi, lakini nina uhakika, kwa asilimia zaidi ya 80, wanawake wanaongea mambo yasiyowasaidia, yaani huyu ana vile, yule ana hivi, wale wanafanya hivi na mambo mengine kama hayo.
Usiwasikilize na kuwaamini. Jione kama uko peke yako na kila anayekuzunguka ni adui. Kuwa makini na unachokiongea mbele yao, na usiwe wakala wa kusambaza kinachozungumzwa nao. Ukiwa hivi, utajiweka salama.
Na hata ukiletewa umbeya, kwamba unasemwa vibaya na huyu, usiwe na haraka ya kuamua mambo, wakati mwingine kusemwa vibaya na kuyaacha kama yalivyo ni baraka.Ila nikusisitize kitu kimoja, mwanamke ana nafasi kubwa zaidi ya kufanikiwa kimaisha duniani kuliko mwanaume, kwa sababu amepewa kila kitu, hasa uwezo wake wa kumshawishi mwanaume amsaidie kufikia ndoto zake!

Post a Comment

أحدث أقدم