WAKATI mambo yakiwa bado tete juu ya afya ya kiongozi wa Kanisa la
Ufufuo na Uzima la jijini Dar es Salaam, Mchungaji Josephat Gwajima,
wafuasi wake wametangaza kufunga kwa muda wa siku 40 kuanzia juzi
Jumatatu ili kuomba.
Mchungaji Josephat Gwajima akiwa hospitali.
Chanzo kilicho ndani ya kanisa hilo ambalo kwa sasa makao makuu yake
yapo Kawe, kililiambia gazeti hili kuwa wafuasi hao wameamua kuliacha
suala hilo mikononi mwa Mungu, hivyo wameona ni vyema kufunga kwa muda
huo ili kumuombea kiongozi wao apate afya njema, lakini pia misukosuko
inayomuandama imalizike.
“Jamaa wameona hali sasa inakuwa ngumu, wanafunga kwa vikundi, kila
mmoja anamuombea apate afya njema baada ya kuzidiwa wakati akihojiwa,
lakini pia wanataka haya mambo yamalizike, kwa hiyo wameona ni bora
kumuachia Mwenyezi Mungu ili ayamalize,” kilisema chanzo hicho.
Mmoja wa wachungaji viongozi wa kanisa hilo aliyeulizwa na gazeti
hili juu ya jambo hilo, huku akitaka jina lake lihifadhiwe kwa vile siyo
msemaji, alikiri waumini kuamua kufunga kwa vikundi, wakiomba katika
maeneo yao ili afya na matatizo ya kiongozi wao yaishe haraka.
Waumini.
Mchungaji Gwajima alianguka ghafla wakati akihojiwa na maofisa wa
Polisi wa Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam, kufuatia maneno yake ya
kashfa dhidi ya Askofu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarb
Kardinali Pengo.
Baada ya kuanguka, mchungaji huyo amekuwa akitibiwa katika Hospitali
ya TMJ iliyopo Mikocheni ambako hali yake imeelezwa kuwa bado tete, huku
kukiwa na taarifa za kukamatwa kwa watu 15 wanaodaiwa kupanga mipango
ya kumtorosha kiongozi huyo wa kiroho kutoka mikononi mwa polisi
wanaomlinda.
إرسال تعليق