Yanga akili nyingi

Wachezaji wa Yanga.
YANGA imekanyaga ardhi ya Zimbabwe na kuitikisa kwa kuwa kila kona ya Mji wa Bulawayo wanaizungumzia mechi yao ya Kombe la Shirikisho dhidi ya FC Platinum.
Yanga wametua huku wakionyesha wao ni wazoefu wa michuano wa kimataifa na wana akili nyingi ya kung’amua mambo kadhaa ambayo waliwekewa kama mtego na wapinzani wao FC Platinum waliowabutua kwa mabao 5-1 jijini Dar.
FC Platinum wanahaha kila sehemu kabla ya mechi ya leo itakayopigwa katika mji wa madini wa Zvishavane ambao uko takribani Kilomita 200 kutoka hapa Bulawayo.Yanga walitua hapa saa tisa jioni na ndege inayomilikiwa na Serikali ya Tanzania na kupokelewa na mashabiki waliotangulia hapa wakiwa wanaongozwa na  Katibu wa Baraza la Wazee Yanga, Mzee Ibrahim Akilimali na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Jerry Muro.
Mara baada ya kutoka nje ya uwanja, walipitiliza moja kwa moja hadi katika basi lililowaleta mashabiki kutoka jijini Dar na kuacha mabasi mawili yaliyokuwa uwanjani pale.Angalia walichokifanya Yanga. Wakati FC Platinum walileta basi lao, Yanga walileta basi jingine walilolikodi na kulilinda kwa siku kadhaa kwa kuwa ndiyo wangetumia wachezaji.
Lakini baada ya kufika, mabasi yote mawili wakaachana nayo na kupanda lile la mashabiki huku mashabiki wakipanda la wachezaji.Mzee Akilimali naye akatoa mpya baada ya kuanza kumwaga maji ‘fulani’ katika eneo la basi wanalopanda wachezaji, mwisho akawazuia kutoa mikono yao kwa mtu yeyote yule.
Ukiachana na basi, Yanga walikataa chakula kilichopikwa katika hoteli ya nyota tano ya Holiday Inn iliyo mjini hapa na kwenda kula kile maalum kilichopikwa na Watanzania.FC Platinum hawakuchoka, waliendelea kufanya ushushu kwa kutuma watu waliofika uwanja wa ndege na kujaribu kufanya uchunguzi lakini hawakuambulia kitu.
Hasira zao zikaishia kwa waandishi wa habari, wakitaka kuwajua ili wawaondoe na ikiwezekana kuwarudisha Tanzania, lakini umafia mwingine ukafanyika kwa kuwavisha jezi za Yanga kuonyesha kuwa ni mashabiki.
Juhudi za FC Platinum kutaka kulipa kisasi cha kutundikwa mabao 5-1 zimekuwa kubwa, lakini wanaonekana kupania kuanza kuucheza mpira nje ya uwanja.

Post a Comment

Previous Post Next Post