Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amesema
endapo vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)
vitashindwa kuafikiana katika kuachiana baadhi ya majimbo kabla ya
Uchaguzi Mkuu, watawaeleza wananchi kwa kuwa ndiyo kiini cha kuanzishwa
kwa umoja huo.
Dk Slaa alisema hayo jana kabla ya kumalizika kwa
vikao vya wakuu wa Ukawa ambao wamekubaliana kusimamisha mgombea mmoja
kuanzia ngazi ya urais, ubunge na udiwani na kwa siku mbili kuanzia
juzi, walikuwa wakijadili ufanikishwaji wa azimio hilo.
Dk Slaa alisema hadi sasa wameshakubaliana
kuachiana asilimia 95 ya majimbo yote na kwamba ana matumaini
watafanikisha, lakini akaonya kuwa ikishindikana, hawatasita kuwaeleza
wananchi.
Mkoani Dar es Salaam, Ukawa imeshafikia muafaka
katika majimbo mawili ya Kawe na Ubungo na kubakiza majimbo sita, wakati
majimbo matano ya mikoa mingine bado yanaupasua kichwa umoja huo wa
vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF na NLD.
“(Kuanzishwa kwa) Ukawa ilikuwa ni ombi la
Watanzania, ni sauti yao kwa hivyo taarifa zinazoendelea kutolewa siyo
sahihi,” alisema akirejea habari kuwa Ukawa, iliyoanzishwa wakati wa
Bunge la Katiba inaelekea kusambaratika kutokana na kushindwa kuafikiana
kwenye baadhi ya majimbo.
“Kama ikitokea tumeshindwa kufikia makubaliano
mwisho wa safari yetu, hakuna kitakachokuwa siri, tutawaeleza
Watanzania,” alisema Dk Slaa.
Hata hivyo, alisema mpaka sasa hakuna dalili
zozote za umoja huo kushindwa kuafikiana kwa sababu ya mvutano wa
majimbo hayo, kwani mpaka sasa wameshafanikiwa kuyagawana kwa asilimia
95 nchini kote.
Alipoulizwa itakuwaje kama hawatafikia muafaka
kwenye vikao hivyo vya siku mbili, Dk Slaa alisema bado kutakuwa na
nafasi ya kuendelea na majadiliano katika vikao vingine.
“Aliyekwambia tuna ratiba ya kumaliza leo (jana)
juu ya mgwanyo wa majimbo hayo ni nani? Hatuna ratiba maalumu kwa kuwa
tunapanga ratiba wenyewe,” alisema Dk Slaa, ambaye ni mmoja wa watu
wanaotajwa kugombea urais kwa tiketi ya Ukawa.
“Kuna mtu mwingine ambaye majadiliano yanapokuwa kwenye hali ya kuvutana, yeye anaona ni mpasuko. Sasa hilo ni tatizo kubwa.”
Habari za ndani kutoka katika vikao hivyo
zinaeleza kuwa uliibuka mvutano mkali kuhusu mgawanyo wa majimbo 17
yaliyobaki mpaka sasa.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi James Mbatia alisema haoni dalili zozote za Ukawa kutofanikiwa katika asilimia tano zilizobakia.
Post a Comment