Dk Slaa: Tutawarejeshea wananchi majimbo tata

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amesema endapo vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vitashindwa kuafikiana katika kuachiana baadhi ya majimbo kabla ya Uchaguzi Mkuu, watawaeleza wananchi kwa kuwa ndiyo kiini cha kuanzishwa kwa umoja huo.
Dk Slaa alisema hayo jana kabla ya kumalizika kwa vikao vya wakuu wa Ukawa ambao wamekubaliana kusimamisha mgombea mmoja kuanzia ngazi ya urais, ubunge na udiwani na kwa siku mbili kuanzia juzi, walikuwa wakijadili ufanikishwaji wa azimio hilo.
Dk Slaa alisema hadi sasa wameshakubaliana kuachiana asilimia 95 ya majimbo yote na kwamba ana matumaini watafanikisha, lakini akaonya kuwa ikishindikana, hawatasita kuwaeleza wananchi.
Mkoani Dar es Salaam, Ukawa imeshafikia muafaka katika majimbo mawili ya Kawe na Ubungo na kubakiza majimbo sita, wakati majimbo matano ya mikoa mingine bado yanaupasua kichwa umoja huo wa vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF na NLD.
“(Kuanzishwa kwa) Ukawa ilikuwa ni ombi la Watanzania, ni sauti yao kwa hivyo taarifa zinazoendelea kutolewa siyo sahihi,” alisema akirejea habari kuwa Ukawa, iliyoanzishwa wakati wa Bunge la Katiba inaelekea kusambaratika kutokana na kushindwa kuafikiana kwenye baadhi ya majimbo.
“Kama ikitokea tumeshindwa kufikia makubaliano mwisho wa safari yetu, hakuna kitakachokuwa siri, tutawaeleza Watanzania,” alisema Dk Slaa.
Hata hivyo, alisema mpaka sasa hakuna dalili zozote za umoja huo kushindwa kuafikiana kwa sababu ya mvutano wa majimbo hayo, kwani mpaka sasa wameshafanikiwa kuyagawana kwa asilimia 95 nchini kote.
Alipoulizwa itakuwaje kama hawatafikia muafaka kwenye vikao hivyo vya siku mbili, Dk Slaa alisema bado kutakuwa na nafasi ya kuendelea na majadiliano katika vikao vingine.
“Aliyekwambia tuna ratiba ya kumaliza leo (jana) juu ya mgwanyo wa majimbo hayo ni nani? Hatuna ratiba maalumu kwa kuwa tunapanga ratiba wenyewe,” alisema Dk Slaa, ambaye ni mmoja wa watu wanaotajwa kugombea urais kwa tiketi ya Ukawa.
“Kuna mtu mwingine ambaye majadiliano yanapokuwa kwenye hali ya kuvutana, yeye anaona ni mpasuko. Sasa hilo ni tatizo kubwa.”
Habari za ndani kutoka katika vikao hivyo zinaeleza kuwa uliibuka mvutano mkali kuhusu mgawanyo wa majimbo 17 yaliyobaki mpaka sasa.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi James Mbatia alisema haoni dalili zozote za Ukawa kutofanikiwa katika asilimia tano zilizobakia.

Post a Comment

أحدث أقدم