Dodoma. Kamati Kuu ya CCM, ambayo ndiyo inaanzisha mambo yote
muhimu ya chama hicho, leo inakutana kuandaa ajenda za mkutano wa
Halmashauri Kuu, huku suala linalosubiriwa kwa hamu likiwa ni hatima ya
makada sita wanaotajwa kuwania urais ambao wanatumikia adhabu ya kuzuiwa
kujihusisha na uchaguzi.
Kwa mara ya kwanza, CCM inakabiliwa na kazi ngumu
ya kuamua hatima ya makada iliowafungiwa katika kipindi muhimu cha
kuteua mgombea mpya wa urais kutokana na mwenyekiti wa sasa wa chama
hicho, Jakaya Kikwete kutoweza kugombea nafasi hiyo kwa kipindi cha tatu
kutokana na matakwa ya kikatiba.
Mmoja wa watu walio karibu na uongozi wa chama
hicho aliiambia Mwananchi jana kuwa CCM imejikita zaidi katika kutafuta
mwanachama atakayekipa ushindi kwenye Uchaguzi Mkuu, lakini suala la
makada waliofungiwa ambao baadhi yao wanapewa nafasi kubwa ya
kupitishwa, halitachukua muda mrefu kulijadili.
Kikao hicho kitafanyika kwenye ukumbi wa
Halmashauri Kuu uliopo jengo la makao makuu ya CCM mjini hapa, maarufu
kama White House mjini Dodoma.
Ukumbi huo una historia ya muda mrefu ndani ya CCM
ya kutolewa kwa uamuzi mgumu katika matukio kadhaa ya kisiasa, ukiwamo
ule ulioweka historia ya Aboud Jumbe kuingia akiwa Rais wa Zanzibar na
mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, lakini akatoka bila cheo chochote
mwaka 1984.
Pia kwenye ukumbi huo kulifanyika uamuzi wa mambo
mengine makubwa, hasa nyakati za kuchuja wagombea urais au uongozi wa
chama, mambo ambayo pia yanaweza kutokea katika vikao vinavyoanza leo au
vya baadaye.
Alipoulizwa kuhusu kikao hicho jana, katibu wa
itikadi na uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema Rais Kikwete ataongoza
kikao cha leo kilichopangwa kuanzia saa 4:00 asubuhi na kwamba
maandalizi yamekamilika, huku baadhi ya wajumbe wakiwa wameshawasili.
Alipoulizwa kuhusu nini wategemee wanachama na
wananchi, Nape alijibu kwa kifupi kuwa watarajie kuwa “CCM watatoka
wakiwa kitu kimoja” kuliko inavyotarajiwa na wengi.
Hata hivyo, mbali na hofu kuhusu hatua za
kinidhamu kwa wajumbe walioadhibiwa kwa kuanza kampeni mapema na kukiuka
maadili, taarifa nyingine kutoka kwa baadhi ya wajumbe wa vikao hivyo
zilidai kuwa mkutano huo utajikita zaidi kuangalia utaratibu mzima wa
kuchukua fomu za wagombea wote wa urais, ubunge na udiwani.
“Vikao hivi vinaangalia utaratibu tu wa jinsi ya
kuchukua fomu na wala havitagusia suala la mchujo wa wagombea urais wala
ubunge,” alisema mtoa taarifa huyo.
Kamati Kuu imetanguliwa na vikao vya mfululizo vya Sekretarieti na Kamati ndogo ya Kanuni.
Kamati ya Kanuni na Maadili ilitarajiwa kukutana jana usiku au leo asubuhi kabla ya Kamati Kuu.
Post a Comment