Ni uamuzi mgumu, ndivyo unavyoweza kusema wakati Kamati Kuu ya Chama
Cha Mapinduzi (CC) inapoanza vikao vya juu mjini Dodoma leo.
Vikao hivyo ni mwelekeo wa chama kuelekea uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani, unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.
Kikao cha kamati hiyo kinatarajiwa kuanza saa nne asubuhi, ambapo
wajumbe wa kikao hicho watajadili masuala mbalimbali, ikiwamo hatima ya
makada sita wa chama hicho waliofungiwa.
Hata hivyo, taarifa ambazo zimetufikia zinasema Kamati ya
Maadili inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Philip
Mangula, ilikutana jana asubuhi kuanzia saa nne hadi saa kumi jioni.
Wakati vikao hivyo vikianza, baadhi ya wapambe wa wagombea urais,
hususan makada sita waliofungiwa waliotua Dodoma kufuatilia vikao,
wamekuwa na hofu iwapo wagombea wao watatoka kifungoni au la.
Mjumbe mmoja ambaye hakutaka jina liandikwe amedokeza kuhusiana na kikao hicho na kueleza kuwa kilichukua muda mrefu
kutokana na uzito wa ajenda.
Mbali ya suala la makada sita, mjumbe huyo alisema baadhi ya makatibu wa
chama wa mikoa na wilaya ambao walilalamikiwa katika kamati hiyo na
baadhi ya wanaCCM kutokana na kukiuka taratibu za chama kwa kuanza
kuwafanyia kampeni wabunge nao walihojiwa.
Mtoa taarifa huyo alisema baada ya kamati kumaliza kikao chake, Kamati
ya Sekretarieti nayo ilikutana jana jioni kuendelea na vikao vyake
vilivyoanza tangu juzi, kwa ajili ya kumalizia ajenda zitakazowasilishwa
katika mkutano wa leo.
Kikao hicho kinatarajiwa kufanyika chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais
Jakaya Kikwete ambapo pamoja na mambo mengine, kitapitisha ajenda
zitakazojadiliwa katika vikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho (NEC),
vitakavyofanyika kesho na keshokutwa.
Kwa upande wake, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, aliwataka
wananchi kupunguza wasiwasi juu ya vikao hivyo na kueleza kuwa chama
hicho kitamaliza vikao vyake salama na wajumbe watatoka wamoja na nguvu
kubwa.
Nape
alitoa taarifa hiyo jana jioni viwanja vya jengo la makao makuu (White
House). Alisema maandalizi kwa ajili ya CC na NEC yamekamilika.
Nape alisema baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu walianza kuwasili tangu
jana jioni, huku wajumbe wa NEC wakiendelea kuwasili tayari kwa ajili ya
vikao vya chombo hicho.
“Tunatarajia baada ya vikao hivi tutatoka Dodoma tukiwa wamoja na wenye
nguvu tofauti na baadhi ya watu wengine wanavyotarajia,” alisema.
Akizungumzia vikao hivyo, Mkuu wa Utawala Ofisi Ndogo na Mjumbe wa NEC
Zanzibar, Bakar Hamad Hamis, alisema matumaini yake ni kupata ajenda
zitakazowaunganisha wana CCM.
“Tangu juzi kulikuwa na vikao mbalimbali vya maandalizi, ikiwamo
sekretarieti, kamati ya masuala ya kanuni na ilani ambavyo viliendelea
hadi jana jioni,” alisema.
Katika maeneo ya jengo la makao makuu ya CCM, kumekuwa na pilikapilika
za wanachama na wasiokuwa wanachama wa CCM ambao wamekuwa wakijadili
mustakabali wa vikao hivyo.
Mbali na hilo, wajasiriamali nao kama kawaida hawakubaki nyuma, kutokana
na kupanga biashara zao, hususan sare za CCM, wakitumia vizuri fursa za
vikao hivyo.
Wanachama wa CCM wamekuwa wakitega sikio Dodoma, kwani vikao hivyo
ndivyo vinavyotarajiwa kutoa dira namna kitakavyowapata wagombea wake
kwa nafasi ya urais, ubunge na udiwani.
Miongoni mwa ajenda zilizojadiliwa katika vikao vya sekretarieti ni
pamoja na maboresho ya mfumo wa kura za maoni, utakaotumika katika
kuwapata wagombea wa chama hicho kwa ajili ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa
kufanyika Oktoba, mwaka huu.
Itakumbukwa Februari, mwaka jana, CCM ilitoa adhabu ya kifungo kwa
makada wake sita waliopatikana na hatia ya kuanza kampeni za urais kabla
ya wakati, kinyume cha maadili na kanuni za chama hicho.
Makanda hao ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira,
Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, Naibu Waziri wa Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia, January Makamba, Mbunge wa Monduli, Edward
Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard
Membe na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.
Lakini hadi jana mchana, Kamati ya Maadili ilikuwa haijakaa na kuandaa ripoti yake.
Kamati ndogo ya kuwachunguza inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa
CCM-Bara, Philip Mangula, inatarajiwa kuwasilisha taarifa yake.
Chanzo chetu kutoka Dodoma kilisema: “Kaka nakwambia mambo yote sawa,
lakini macho na masikio yako kwenye Kamati ya Maadili, hii ndiyo imebeba
roho zetu hapa mjini.
“Tunaweza kutoka tunachekelea au tumenuna…si unajua inakuja na hukumu ya
makada sita, tuwe wavumilivu mambo yanaanza kesho (leo).
“Kila kona ya mji huu tunahemea juujuu utafikiri bundi asiyekuwa na
pumzi…lakini Mungu ni mwema, naamini atutusaidia ili tuvuke jahazi hili
salama,” kilisema chanzo chetu.
Chanzo: Mtanzania
Post a Comment