JB: NILILELEWA ‘KI-MAMA’ MAMA SANA!

 
Msanii nguli kwa sasa katika tasnia ya filamu Bongo, Jacob Steven Mbura ‘JB’.
MKONO mmoja ulikuwa shavuni nikiendelea kusoma kitabu kipya cha ujasiriamali kilichoandikwa na mhamasishaji nguli barani Afrika wa watu kujikomboa na umasikini, Eric Shigongo kiitwacho Jinsi ya Kutoka Kwenye Umasikini Hadi Mafanikio kinachopatikana mitaani kwa bei nafuu, nikiinua kichwa mara kwa mara na kuangaza macho huku na kule nikimsubiri mtu aliyenifanya niwe katika eneo hilo. Ndiyo, sikuwa nimechelewa wala kuwahi sana, nilikuwa hapo kwa wakati.
Nilikuwa ndani ya viwanja vya Leaders Club, Kinondoni jijini Dar, nikimngoja kwa hamu msanii nguli kwa sasa katika tasnia ya filamu Bongo, Jacob Steven Mbura ‘JB’. Lengo likiwa ni moja tu. Kupata simulizi ya maisha yake tangu anazaliwa hadi alipo sasa.

Sikujishughulisha sana na magari yaliyokuwa yakiingia uwanjani hapo, lakini ghafla nililazimika kusitisha kila kitu baada ya kuingia gari ambalo kila aliyekuwa maeneo hayo alilikazia macho.
Ndiyo, ilikuwa ni Toyota, Land Cruiser VX-V8. Halikushangaza wengi kwa aina yake, bali kwa rangi ya mng’aro lililonakshiwa.
Baada ya salamu, mazungumzo yakachukua nafasi huku nikiwa na shauku kubwa ya kujua maisha halisi ya gwiji huyu wa sanaa kwa sasa! Haraka sana naikamata na kuikaza vyema kalamu yangu na kuanza kudondosha wino kwa kila elezo alilolisema. Ungana nami katika simulizi hii tamu ya maisha halisi ya JB.
KUZALIWA
JB alizaliwa katika Hospitali ya Ocean Road jijini Dar, miaka kadhaa iliyopita, wakati huo familia ikiishi Mwananyamala. Familia ya JB ilikuwa na uchumi wa wastani kutokana na wazazi wake kuwa watumishi wa serikali jambo lililorahisisha malezi yake.
MAISHA YA UTOTONI
Wakati JB akiendelea na simulizi, ghafla namuona akigeuza shingo pembeni na kukazia macho mahali fulani. Taratibu naamua kutazama eneo ambalo alilikazia macho. Alikuwa  akimtazama mhudumu wa vinywaji na chakula, haraka sana anamuita na kumwagizia vinywaji pamoja na oda ya msosi.
“Unajua (akilitaja jina la mwandishi) usione nina mwili kama huu, afya haiboreshwi kwa udongo na matofali bali kwa chakula, ngoja tule kwanza huku mazungumzo yakiendelea,” anasema huku akinitazama na kuachia kicheko kilichowafanya watu wote waliokuwa eneo hilo wageuke na kututazama.
JB anasema maisha yake ya utotoni hayakuwa na fujo nyingi sana kama ilivyo kwa watoto wengi kwani alikuwa mpole na mkimya. Muda mwingi aliutumia kuwa kimya na wakati mwingine kujitenga na watoto wenzake hasa kunapokuwa na kelele nyingi.
“Nilikuwa mkimya na mpole sana, maisha yangu ya utotoni hayakuwa na fujo nyingi, unajua nililelewa kwa kudekezwa sana, yaani ki-mama mama hivyo nilikuwa muoga, muda mwingi nilikuwa najitenga na wenzangu hasa kama kuna kelele na dalili za ugomvi,” anasema JB huku akikohoa kidogo na kujirekebisha vyema kitini.
ALIPENDELEA MICHEZO GANI?
“Nilipenda sana mchezo wa mpira wa miguu, hadi leo ninapoongea na wewe hapa, hakuna mchezo ninaoupenda kama huo, nilipendelea sana kucheza mpira na watoto wenzangu ambao hawakuwa wakorofi. Mara nyingi niligombana sana na mama kwa kuchelewa kuoga kwa sababu ya mpira,” anasema JB.Wakati JB anaendelea kukumbuka na kusimulia kwa hisia kali maisha michezo aliyoiupendelea utotoni, ghafla..

Post a Comment

أحدث أقدم