Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi
Hatua hiyo inatokana na kubainika kuwapo kwa vifungu vya katiba hizo hasa vinavyohusu uwapo wa vikundi vya ulinzi na usalama na hivyo kukiuka Katiba ya nchi inayotoa haki hiyo kwa majeshi ya ulinzi na usalama.
Taarifa za uhakika zilizopatikana ndani ya ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, zimethibitisha kuwapo upungufu ukiwamo wa sheria inayoviongoza vyama hivyo na uhalali wa kuwapo vikundi hivyo.
Pia vikundi hivyo vinatazamwa kama moja ya upenyo unaoweza kuwajengea uwezo wa kijeshi watu tofauti hasa vijana, kisha wakatumika kwa matendo maovu kama ugaidi na hivyo kuathiri hali ya usalama wa nchi.
Pamoja na kurekebisha katiba za vyama kuhusu vikundi hivyo, taarifa zinaeleza kuwa mpango huo utahusisha kupiga marufuku uwapo wa vikundi hivyo na watakaobainika kuratibu, kusimamia ama kuendesha mafunzo ya vikundi hivyo, atatuhumiwa kwa makosa ya jinai.
Jaji Mutungi, aliithibitishia NIPASHE Jumapili kuhusu mpango wa kuwapo marekebisho ya sheria inayoviongoza vyama vya siasa nchini.
Wakati Jaji Mutungi akithibisha hivyo, vyanzo vyetu vimebaini kuwa mpango wa kuwapo mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa ulianza kuratibiwa na mtangulizi wake, John Tendwa lakini ukapingwa na vyama vya siasa hususani upinzani.
Wapinzani waliupinga mpango huo kwa madai kuwa marekebisho hayo yalilenga kuvidhoofisha na kujenga mazingira ya kukipa nguvu zaidi Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Marekebisho hayo yangefanyika ni dhahiri kwamba angalau kungekuwapo hali nzuri ya kuviendesha vyama hivyo kwa ushindani unaochangia kukuza zaidi demokrasia na misingi ya haki za binadamu,’ kilieleza chanzo chetu.
CCM YAKEMEWA
Ndani ya CCM, taarifa zinaeleza kuwa Jaji Mutungi ameshakutana na viongozi kadhaa wakiwamo wa ngazi ya kitaifa, akiwajulisha hatari iliyopo kwa usalama wa nchi ikiwa vyama vya siasa vitaachwa kuvifanya vikundi vya ulinzi kuwa shughuli halali kwa uendeshaji wao.
Miongoni mwa viongozi wanaotajwa kukutana na Jaji Mutungi kwa nyakati tofauti ni Mwenyekiti wa Taifa, Rais Jakaya Kikwete na Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana.
UHARAMU WA VIKUNDI
Vyanzo vyetu vinaeleza kuwa uendeshaji wa vikundi vya ulinzi na usalama ndani ya vyama vya siasa, japo unatambulika kwa mujibu wa katiba za chama husika, hauna miongozo na kanuni za kisheria kwa mujibu wa Katiba ya nchi.
Hali hiyo inaelezwa kuchangia kwa kiasi kikubwa uwezekano wa vyama kutoa mafunzo yasiyofaa kwa mustakabali wa nchi.
Mafunzo hayo ni pamoja na namna ya kuvamia, kupiga, kujihami ikibidi kuua.
“Ni kutokana na kutokuwapo kanuni na miongozo ya kisheria kwa vikundi hivyo ndio maana hakuna utaratibu ulio sawa katika utoaji mafunzo na uendeshaji wake, hii ni hatari kubwa kwa nchi na watu wake,” chanzo kingine kilieleza.
MBOWE APINGWA
Uhalisia huo unakuwa kinyume na kauli iliyowahi kutolewa hivi karibuni na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe.
Mbowe alisema vikundi hivyo havina madhara wala athari zozote, akifananisha na utendaji kazi wa kampuni binafsi za ulinzi.
Lakini wachambuzi wa masuala ya sheria wameipinga hoja ya Mbowe kwa maelezo kuwa, tofauti na ilivyo kwa vyama vya siasa, kampuni za ulinzi zina sheria na kanuni zinazowaongoza katika utendaji kazi wao.
“Kampuni binafsi za ulinzi zikikiuka sheria na kanuni zilizopo, ni dhahiri kwamba zinaadhibiwa, hivyo sivyo ilivyo kwa vikundi vya ulinzi vya vyama vya siasa,” alieleza mwanasheria mmoja ambaye hakutaka jina lake kutajwa gazetini.
إرسال تعليق